1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama aishutumu Urusi katika mzozo na Ukraine

29 Agosti 2014

Ukraine na mataifa ya magharibi zimesema majeshi ya Urusi yanahusika moja kwa moja katika mapigano yanayolivuruga eneo la mashariki mwa nchi hiyo, na kuzusha hofu ya mapambano ya moja kwa moja kati ya Ukraine na Urusi.

https://p.dw.com/p/1D3Y7
Obama spricht von einem russischen Vormarsch im Osten der Ukraine
Rais Barack Obama wa marekaniPicha: picture-alliance/dpa

Rais wa Marekani Barack Obama ameongoza sauti zinazoongezeka za shutuma za kimataifa kuhusiana na kuongezeka kwa mzozo huo, akisema ni wazi kabisa kwa dunia kuona , kwamba majeshi ya Urusi yanapigana nchini Ukraine, licha ya Urusi kukana mara kwa mara tuhuma hizo.

Obama na kansela wa Ujerumani Angela Merkel wameonya kuwa hatua za Urusi "haziwezi kuendelea bila ya kujibiwa", wakati Marekani na mataifa ya Ulaya yakiongeza uwezekano wa vikwazo vipya dhidi ya nchi hiyo.

Westbalkan-Konferenz
Kansela Angela Merkel wa UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa

"Urusi kwa makusudi kabisa imerudia kukiuka tena mipaka na uhuru wa Ukraine, na picha mpya zinazoonesha majeshi ya Urusi ndani ya Ukraine zinaweka wazi kila kitu kwa dunia kuona'', Obama amesema , akiongeza mbinyo dhidi ya rais wa Urusi Vladimir Putin.

Jumuiya ya kujihami ya NATO imesema kiasi wanajeshi 1,000 wa Urusi wako ndani ya Ukraine wakiwasaidia wapiganaji wanaounga mkono Urusi ambao wamekuwa wakipambana dhidi ya utawala wa Kiev tangu mwezi Aprili.

Brigadia jenerali wa NATO kutoka Uholanzi Nico Tak hakutaka kuzungumzia kuhusu Urusi kuivamia Ukraine , lakini amesema hali inazidi kuwa mbaya.

"Katika wiki mbili zilizopita tumegundua kuongezeka mno kwa kiwango na mbinu za hali ya juu za uingiliaji kijeshi wa Urusi ndani ya Ukraine. Picha za satalaiti zilizoonekana leo zinatoa ushahidi kuwa wanajeshi wa Urusi wenye silaha za kisasa wako ndani ya ardhi ya Ukraine."

NATO General Nico Tak PK SHAPE Mons 28.08.2014
Brigadie jenerali wa NATO Nico Tak kutoka UholanziPicha: Reuters

Marekani na Umoja wa Ulaya tayari zimeweka vikwazo dhidi ya Urusi kuhusiana na mzozo huo, ikiwa ni mkwamo mkubwa kati ya Urusi na mataifa ya magharibi tangu kumalizika kwa vita baridi.

Rais Vladimir Putin kwa upande wake amewataka wapiganaji wanaotaka kujitenga wanaounga mkono Urusi nchini Ukraine kuweka eneo linaloitwa la kiutu," kuwaruhusu wanajeshi wa serikali ya Ukraine ambao wamezingirwa kurudi nyuma.

Wapiganaji wa jeshi la serikali ya Ukraine ambao wamezingirwa wamekuwa wakipambana wakitapia maisha yao katika mji wa Ilovaysk kwa zaidi ya wiki sasa wakati waasi wanaoiunga mkono Urusi ambao wamekuwa wakirudi nyuma , walipoanza kufanya mashambulizi ya kushitukiza.

Putin amewaeleza wapiganaji hao moja kwa moja kuwa wanatetea , Novorossiya , ama Urusi mpya, neno lililokuwa likitumiwa na watawala wa kifalme wa zamani wakati wakiwania kupanua himaya yao.

Putin PK in Minsk 27.08.2014
Rais Vladimir Putin wa UrusiPicha: Reuters/Alexei Druzhinin/RIA Novosti

Rais Barack Obama ametoa onyo kwa Urusi kutokana na uingiliaji huo.

"Ukraine sio mwanachama wa NATO. Lakini mataifa kadhaa ya jirani ni wanachama. Na tunaichukulia ibara ya tano inayotulazimu kuwalinda wanachama kwa umuhimu wa juu kabisa."

Rais Petro Poroshenko wa Ukraine ameitisha mkutano wa dharura wa wakuu wa usalama jana kuweka miakakati juu ya vipi kuchukua hatua dhidi ya mafanikio ya haraka ya wapiganaji kusini mwa jimbo la Donetsk mashariki mwa Ukraine.

Ameuambia mkutano huo kuwa hali ni ngumu mno, lakini inayoweza kudhibitiwa " baada ya wapiganaji wanaoungwa mkono na Urusi kukamata mji wa Novoazovsk upande wa kusini mashariki, katika pwani ya bahari ya Azov.

Petro Poroschenko
Rais Petro Poroshenko wa UkrainePicha: Reuters

Hapo mapema Poroshenko amesema amefuta ziara nchini Uturuki kwasababu ya hali inayoporomoka kwa haraka , katika jimbo la mashariki la Donetsk , "wakati majeshi ya Urusi yameingizwa sasa katika ardhi ya Ukraine.

Wizara ya ulinzi ya Urusi kwa mara nyingine tena imekana kuwapo kwa wanajeshi wake nchini Ukraine, ikitumia lugha ya wakati wa vita baridi.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe

Mhariri:Gakuba Daniel