Obama ahimiza ushirikiano mpya na China
8 Juni 2013Obama alikiri kuwa kuna masuala yanayopingana kati ya mataifa hayo mawili, ikiwa ni pamoja na udukuzi katika mtandao wa internet na masuala ya kibiashara, lakini amesisitiza kuwa kuna maeneo kadha ambayo nchi hizo mbili zinaweza kushirikiana.
"Hakuna shaka kuwa kuna maeneo yanayoleta mivutano baina ya nchi zetu mbili, lakini kile nilichojifunza katika muda wa miaka minne iliyopita ni kwamba watu wa China na Wamarekani wanataka uhusiano imara wa ushirikiano ," Obama amesema.
Marais watambua
Kuna hali ya kutambua kwa upande wa marais wote Xi na mimi binafsi kuwa ni katika maslahi ya nchi zetu kufanya kazi kwa pamoja kupambana na changamoto za dunia ambazo tunakabiliwa nazo."
Xi ameyaita mazungumzo hayo "sehemu ya kihistoria ya kuanzia," akidokeza kuwa kukutana muda mfupi tu baada ya yeye kuchukua madaraka mwezi Machi kunaashiria umuhimu wa mahusiano ya nchi hizo mbili.
"Wakati nilipotembelea Marekani mwaka uliopita, nilisema kuwa bahari kubwa ya Pacific ina nafasi ya kutosha kwa mataifa haya mawili ya China na Marekani. Bado naamini hivyo," Xi amesema.
Wakati wanajaribu kuleta uhusiano mpya wa mataifa hayo makubwa yenye nguvu , vikwazo kama shutuma za Marekani kuhusu udukuzi katika mtandao wa internet kuhusiana na miundombinu ya kijeshi na wizi wa mbinu za kutengeneza bidhaa zinaweza kurejesha hali ya kutoaminiana.
Viongozi hao wawili wanatarajiwa kujadili masuala kadha kuanzia matatizo ya uimarishaji wa mikakati yao ya uhasama hadi katika mahusiano ya kibiashara pamoja na mpango wa kinuklia wa Korea ya kaskazini.
"Marekani inakaribisha China inayoinukia kwa amani kama taifa lenye nguvu duniani," Obama amesema. "Kwa hakika , ni kwa maslahi ya Marekani kwamba China inaendelea katika njia ya mafanikio."
Hakuona haya hata hivyo kutaja wasi wasi wa Marekani juu ya usalama katika mtandao wa internet, na haki za binadamu nchini China pamoja na umuhimu wa biashara huru na ya haki.
Udukuzi katika mtandao
Mashambulizi katika mtandao wa internet ni suala linaloongeza wasi wasi kwa umma wa Marekani baada ya ripoti ya hivi karibuni ya serikali kudai kuwa kuna mashambulizi kutoka China dhidi ya miundo mbinu ya jeshi na biashara. Wiki iliyopita , waziri wa ulinzi Chuck Hagel ameyaita mashambulio hayo kuwa yanaleta wasi wasi katika jeshi na yanahitaji kushughulikiwa haraka iwezekanavyo.
Maafisa wa Marekani wana matumaini suala hilo halitatawala majadiliano ya marais hao, yakielekea zaidi katika masuala kama mpango wa Korea ya kaskazini wa kinuklia, mizozo ya kuwania maeneo ya ardhi katika eneo kuzunguka mataifa karibu na China na wasi wasi wa Marekani juu ya haki za binadamu nchini China. Obama pia ana matumaini kujifunza mengi juu ya mageuzi ya kiuchumi ndani ya China yanayotarajiwa kufanywa na rais Xi.
China inatarajia ziara ya Xi kulenga katika kujenga mahusiano na Obama, pamoja na masuala muhimu maalum ambayo Obama huenda atayaweka mbele ya mazungumzo hayo , kama usalama wa mtandao wa internet, Korea ya kaskazini , na mvutano wa hivi karibuni kati ya China na Japan kuhusiana na visiwa vinavyogombaniwa na mataifa hayo.
Mwandishi : Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Daniel Gakuba