1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama afupisha kifungo cha mvujisha siri za Marekani

Isaac Gamba
18 Januari 2017

Rais Barack Obama  amefupisha kifungo gerezani  cha mchambuzi wazamani wa masuala ya kijasusi wa Marekani Chelsea Manning ambaye alihusika na uvujishaji wa taarifa za siri kwa mtandao wa WikiLeaks mwaka 2010.

https://p.dw.com/p/2VyM8
USA Chelsea Manning Transgender Soldat
Picha: picture-alliance/AP Photo/U.S. Army

Afisa wa  ikulu ya  Marekani amesema  kufipishwa  kifungo hicho hakuhusiani  na hatua ya sasa ya Marekani ya  kuhusishwa  tena mtandao wa WikiLeaks katika uchaguzi wa Marekani wa mwaka jana ama ahadi ya muasisi wa mtandao huo Julian Assange ya kukubali kupelekwa Marekani iwapo Manning angeachiwa huru.

 Manning aliibua mjadala mkubwa kimataifa  kutokana na kitendo chake cha kuvujisha siri za serikali kwa mtandao wa WikiLeaks akitoa nyaraka 700,000 za siri , mikanda ya vidio ya taarifa za serikali na taarifa za siri za kivita hali iliyopelekea ahukumiwe kifungo cha miaka 35 gerezani.

Rais Barack Obama katika moja ya hatua zake za hivi karibuni kabla ya kuondoka madarakani ameamua kufupisha kifungo cha Manning hadi miaka saba hatua ambayo imeonekana kuwakasilisha warepublican.

Spika wa bunge la wawakilishi Paul Ryan katika taarifa yake amelaumu uamuzi huo akisema ni hatari hasa kuhusiana na kuwapa nafuu wale ambao wanavujisha taarifa nyeti za serikali.

Manning alikuwa akifanya kazi kama mchambuzi wa masuala ya kijasusi mjini Baghdad mnamo mwaka 2010 wakati alipovujisha taarifa za siri za kivita ikiwa ni pamoja na mkanda wa vidio ulionyesha  helikopta ya kivita ya Marekani ikishambulia washukiwa wa uasi dhidi ya serikali ya Iraq  ambapo watu kadhaa waliuawa wakiwemo waandishi wa habari wawili wa shirika la habari la Reuters.

Seneta wa Republican Tom Cotton amesema kuvujishwa kwa taarifa hizo za siri zilileta hatari kubwa kwa wanajeshi wa Marekani, maafisa wa kijasusi, wanadiplomasia pamoja na washirika wao.

Manning aishi kama mwanamke wa jinsia mbili

Manning  alizaliwa kama mwanaume lakini baada ya kutiwa hatiani alijitambulisha kuwa ni mwanamke.   Ikulu ya White House imesema kifungo chake kitafikia mwisho May 17 mwaka huu.

Manning  ambaye amekuwa akipambana kuishi kama mwanamke mwenye jinsia mbili na huku pia akijaribu mara mbili kutaka kujiua katika gereza la wanaume la Fort Leavenworth, Kansas alikubali kuvujisha taarifa hizo za siri hatua ambayo inaelezwa kuchangia uamuzi wa Rais Barack Obama wa kufupisha kifungo chake.

 

USA Präsident Barack Obama Abschiedsrede in Chicago
Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: Picture-Alliance/AP Photo/P. Ma. Monsivais

Mmoja wa maafisa wa Ikulu ya Marekani ambaye hakutaka kutajwa jina  amesema  uamuzi huo wa Obama umezingatia kifungo cha Manning kuwa kirefu zaidi ukilinganisha na  vifungo vinavyotolewa kwa watu wengine waliofanya uhalifu wa aina hiyo.

Hata hivyo Ikulu  imesema uamuzi huo wa Rais Obama hauhusiani na hatua ya sasa ya WikiLeaks ambapo imekuwa ikihusishwa na kuchapisha barua pepe wiki chache kabla ya uchaguzi wa Novemba 8, mwaka jana hatua ambayo mashirika ya kijasusi ya Marekani yanaamini kuwa ilichangia pia Urusi kuingilia uchaguzi huo kwa lengo la kushawishi matokeo ya uchaguzi huo.

Rais Obama ambaye ataondoka rasimi madarakani Ijumaa wiki hii atafanya  mkutano wake wa mwisho na waandishi wa habari hii leo ambapo pia anatarajiwa kulizungumzia suala hilo.

Mwandishi: Isaac Gamba/ RTRE

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman