1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama aapa kuboresha uhamiaji Marekani

21 Novemba 2014

Rais Barack Obama wa Marekani ameahidi kuifanyia marekebisho sera ya uhamiaji ya nchi hiyo, na kuahidi kuwaepusha hatari ya kufukuzwa - wahamiaji milioni 5 waishio nchini humo kinyume na sheria.

https://p.dw.com/p/1Dqrh
Rais Barack Obama wa Marekani
Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: picture-alliance/dpa/Olivier Douliery

Katika hotuba ya dakika 15 aliyoitoa katika Ikulu ya White House mjini Washington, rais Barack Obama amesema takribani wahamiaji wote wanaoishi nchini humo bila vitambulisho kwa zaidi ya miaka 5 na wale ambao wanao watoto wenye uraia wa Marekani, wanaweza kuomba kibali kitakachowaruhusu kufanya kazi nchini humo kwa muda wa miaka mitatu.

Rais Obama vile vile amepanua mpango mwingine aliouanzisha mwaka 2012, ambao unawapa ruhusa ya muda kuishi nchi Marekani, wahamiaji haramu walioingia nchini humo wakiwa na umri wa chini ya miaka 16. Obama amesema hatua yake hiyo haijakiuka sheria yoyote.

''Hizi ni hatua ambazo ninao uwezo kisheria kuzichukua kama rais. Haina tofauti yoyote na zile zilizochukuliwa na marais walionitangulia, wawe kutoka chama cha Republican, au cha Democratic - kwa lengo la kuuboresha mfumo wetu wa uhamiaji ili uwe wa haki zaidi.'' Amesema rais huyo.

Akosoa unafiki wa mfumo wa sasa

Mpango huu wa Obana utawanufaisha asilimia 44 ya wahamiaji haramu milioni 11.3 waishio nchini Marekani, ambao wengi ni kutoka Mexico na nchi nyingine za Amerika ya Kati, wanaofanya kazi zinazodharauliwa na wamarekani.

Wahamiaji wengi haramu ni wale wanaofanya kazi zinazobezwa na wamarekani
Wahamiaji wengi haramu ni wale wanaofanya kazi zinazobezwa na wamarekaniPicha: picture-alliance/dpa

''Je, sisi ni taifa linalovumilia unafiki wa mfumo ambao unawanyima haki kisheria, watu wanaovuna matunda katika bustani zetu, na wanaotutandikia vitanda?'', aliuliza rais Obama katika hotuba yake hiyo.

Hata hivyo Obama amekumbusha kwamba mpango wake huo hauwapi watu hao uraia wala kibali cha kuishi milele nchini Marekani, akisema ni bunge tu lenye uwezo wa kufanya hivyo.

Chama cha Republican chaapa kumpinga Obama

Wanachama wa chama cha upinzani cha Republican ambacho kwa sasa kinayadhibiti mabaraza yote ya Bunge, wameonya kuwa hatua yoyote kuhusu uhamiaji itakayochukuliwa na rais peke yake, itakuwa kinyume cha sheria.

Akizungumza kabla ya hotuba ya rais Obama jana,Mitch McConnell ambaye atakuwa kiongozi wa maseneta wa chama cha Republican walio wengi katika baraza hilo, amesema ikiwa Obama atakaidi matakwa ya wananchi na kulazimisha matakwa yake juu ya taifa, bunge litachukua hatua.

Mitch McConnel, kiongozi wa maseneta wa Republican amesema watapinga mpango wa Obama
Mitch McConnel, kiongozi wa maseneta wa Republican amesema watapinga mpango wa ObamaPicha: Getty Images/W. McNamee

Kamati ya kitaifa ya chama hicho cha upinzani imeilinganisha hatua hiyo ya Obama na sheria iliyotungwa na mtu mmoja, kutoa msamaha kwa wahamiaji haramu, kinyume cha katiba.

Wahamiaji haramu ambao kulingana na tangazo la Obama wanapaswa kutoka mafichoni na kutafuta kibali cha muda wameupokea kwa wasiwasi wito huo.

Mmoja wao, Norma Martinez kutoka El Salvador, amesema ingawa hapendi kuishi kwa kujifichaficha, anahofia kile kitakachofuata ikiwa atajitokeza, na kisha mpango wa Obama ukaondolewa. ''Bila shaka hatua itakayofuata ni kutufungisha virago na kutimliwa'', amesema mama huyo ambaye amekuwa akiishi nchini Marekani tangu mwaka 2007.

Wataalamu wa sheria vile vile wameonya kwamba ingawa mpango huo wa Obama unachelewesha kufukuzwa kwa wazazi wa watoto wenye uraia wa Marekani, unaambatana na kasoro nyingi ambazo zina uzito mkubwa kuliko faida.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/AFPE

Mhariri:Josephat Charo