Nzige watua Congo
26 Februari 2020Shirika hilo la chakula FAO aidha limeonya juu ya kitisho kikubwa cha njaa katika mataifa ya Afrika Mashariki baada ya kuvamiwa na nzige hao.
Kenya, Somalia na Uganda zimekuwa zikipambana na wadudu hao, katika mripuko mbaya kabisa wa nzige ambao maeneo kadhaa ya ukanda huo yalishuhudia miaka 70 iliyopita. Umoja wa Mataifa umesema nzige hao wa jangwani pia wameonekana Djibout, Eritrea na Tanzania na katika siku za karibuni wamefika Sudan Kusini, taifa ambalo kwa takribani nusu ya idadi ya watu wake tayari wanakabiliwa na njaa baada ya miaka kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa jana jioni na mkurugenzi mkuu wa FAO Qu Dongyu, mkuu wa shirika la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa Mark Lowcock na mkurugenzi mtendaji wa mpango wa chakula duniani, WFP, David Beasley, imefananisha kundi hilo la nzige kama janga la kiwango kilichozungumziwa katika bibilia na linalokumbushia hatari inayoukabili ukanda huo.
Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Stephane Dujarric, akiwa mjini New York hapo jana amezungumza mwito wa ufadhili uliotolewa na FAO wa dola milioni 76 wa kupambana na wadudu hao, ambao hata hivyo unatekelezwa kwa kasi ndogo.
"Maafisa wameomba msaada huo wakati nzige walipoendelea kuvamia kote mashariki mwa Afrika. Gharama za kukabiliana nao zimeongezeka mara mbili hadi dola milioni 138. Mpango wa chakula umeonya gharama za kupambana na athari za nzige kwenye usalama wa chakula tu, zinaweza kuwa mara 15 zaidi ya gharama ya kuwazuia kusambaa. Hadi sasa ni dola milioni 33 tu zimetolewa au kuahidiwa." amesema Dujarric.
FAO imesema nzige waliozeeka , wanaoletwa kwa sehemu na upepo, waliwasili katika pwani magharibi mwa ziwa Albert, karibu na mji wa Bunia mashariki mwa Congo siku ya Ijumaa. Taifa hilo halijawahi kushuhudia nzige kwa miaka 75.
Taarifa hiyo ya pamoja imesema, bila hata ya kugusia kitisho dhahiri kwenye taifa hilo, ambalo bado linakabiliwa na mzozo mgumu, maradhi ya Ebola na mripuko wa surua, kiwango kikubwa cha wakimbizi wa ndani pamoja na usalama duni kabisa wa chakula, ni wazi kuwa hali itakuwa mbaya sana.
Kundi la nzige linaweza kufikia ukubwa wa majiji makubwa na linaweza kuharibu mazao na malisho ya mifugo. Wataalamu wameonya kwamba mripuko wa nzige unaathiri mamilioni ya watu ambao tayari wana hali mbaya kote kwenye ukanda huo.
Serikali ya Uganda imesema jana Jumanne kwamba ilikuwa inajaribu kulidhibiti kundi la nzige na itahitaji rasilimali zaidi za kudhibiti wingi wa wadudu hao ambao wamesambaa kwenye mikoa zaidi ya 20 kaskazini mwa nchi hiyo. Wanajeshi wamekuwa wakikabiliana na nzige hao kwa kutumia dawa za kupuliza kwa mashine zinazotumia mikono, wakati wataalamu wakiwa tayari wamesema suluhu pekee ni dawa hizo kupuliziwa kutoka angani.
Umoja wa Mataifa hivi karibuni umetoa mwito wa ufadhili kutoka dola milioni 76 hadi 138. Wataalamu wameonya iwapo nzige hao hawatashughulikiwa, wataongezeka mara 500 ifikapo mwezi Juni, wakati ambapo kunatarajiwa hali ya hewa ni ya ukavu kwenye ukanda huo.