Nzige wa jangwani wavamia Uganda
10 Februari 2020Makundi mawili ya wadudu hao waharibifu yamegunduliwa eneo la Karamoja nchini Uganda. Serikali ikishirikisha majeshi imewapeleka makundi ya maafisa na wataalamu kupambana na nzige hao.
Katika muda wa saa tatu tu baada ya nzige hao kuonekana mpakani, walikuwa wamefika katika wilaya mbili jirani za Amudat na Nakapiripirit. Kundi hilo la nzige linadhaniwa lilitokea eneo la Pokot Magharibi nchini Kenya.Kwa kuwa nzige hao wanasambaa kwa kasi kubwa, maafisa wa wizara ya kilimo wanasema watalazimika kusambaza vifaa maeneo mbalimbali ili kukabiliana nao.
Mara tu baada ya taarifa za nzige hao kuthibitishwa, makundi ya maafisa na majeshi wamelekwa katika maeneo yaliyovamiwa kwa lengo la kuwanyunyuzia dawa kama hatua ya kwanza kukabiliana nao.
Waziri mkuu Dkt Ruhakana Rugunda ametoa mwito kwa wananchi wote kushiriki katika zoezi la kukabiliana na nzige hao ambao ameelezea kuwa wataathiri upatikanaji wa chakula na uchumi kuanzia ngazi ya familia.
Wizara ya kilimo imefafanua kuwa imekuwa ikijiandaa kukabiliana na uvamizi wa nzige hao kwa muda wa wiki mbili sasa tangu ilipobainika kwamba walikuwa kilomita chache kutoka mpaka wa Uganda na Kenya. Huku akisisitiza kuwa kemikali zinazotumiwa kungamiza nzige hao hazina madhara kwa binadamu, kamishna wa idara ya kulinda mimea Stephen Tibaijuka amelezea kuwa vifaa vyote vinavyohitajika vilikwisha wasilishwa eneo la Karamoja.
Kulingana na shirika la chakula na kilimo duniani uvamizi huu wa nzige ndiyo mbaya zaidi katika kipindi cha miaka 70. Kundi moja la nzige laweza kuharibu chakula cha hadi watu 2,500 kwa siku moja tu, na hujumzuisha wadudu milioni 150 katika eneo la kilomia moja mraba.