Nyota wa Ghana wapepea bendera ya Afrika
24 Juni 2010Hiyo jana, Ujerumani ilinusurika, baada ya kuilaza Ghana kwa bao 1-0 katika mchezo wa kufa kupona, pande hizo mbili zilipokumbana uwanjani Soccer City mjini Johannesburg.
Baada ya kuchuana kwa dakika sitini nzima, Mesut Oezil wa Ujerumani, aliuvurumisha mpira katika wavu wa Ghana na hivyo kuinusuru Ujerumani kufunga virago na kurejea nyumbani katika duru ya mwanzo ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza kabisa.
Hata hivyo, Ghana iliitoa jasho Ujerumani na imethibitisha kuwa wao kweli ni nyota. Ghana ni timu pekee kutoka Afrika kubaki katika kundi la timu 16 za mwisho, katika kinyanganyiro hicho cha Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini. Nyota hao wa Ghana, watakumbana na Marekani jumamosi ijayo. Hiyo jana Marekani iliifunga Algeria bao 1-0 na Australia nayo iliicharaza Serbia mabao 2-1.Uingereza pia hiiyo jana ilinusurika kufunga virago, baada ya kuikandika Slovenia bao 1-0.
Uingereza itateremka tena uwanjani siku ya Jumapili kwa mchezo unaongojewa kwa hamu kubwa. Siku hiyo, Uingereza itakwaruzana na Ujerumani.