Nyongeza mpya ya nauli yaathiri usafari Kisumu
18 Septemba 2023Katika kituo cha magari ya uchukuzi jijini Kisumu, kinachojumuisha wanaosafiri maeneo ya mbali, Nairobi, Mombasa, Busia, Uganda, msongamano wa abiria hushudiwa, hasa mwishoni mwa wiki.
Lakini mara hii, abiria wanaofika katika afisi za magari ya kuelekea jiji kuu la Nairobi wanauliza na kuondoka baada ya kutangaziwa nyongeza mpya ya nauli.
Kabla ya nyongeza hii, magari haya yalikuwa yakitoza shilingi 1,500 kwa abiria, lakini sasa nauliimepandishwa hadi shilingi 1,700. Ni muhimu kubainisha kuwa nauli hii ilikuwa ni baina ya shilingi 1,000 hadi 1,200 kadri bei ya mafuta inavyozidi kubadilika.
"Kuna watu wanakuja wakiondoka, ni kwa sababu wamepandisha bei........."
Katibu wa Muungano wa Wamiliki wa Magari ya Uchukuzi hapa Kisumu, James Ochieng Omwa, anasema bei zisizotabirika za mafuta ya gari zimewaweka njiapanda na hivyo wamelazimika kumlimbikizia abiria uzito wa mzigo huo.
Abiria wabebeshwa mzigo
Kwa mujibu wa Ochieng, mabadiliko katika bei za mafuta ni changamoto kwa biashara zao kwani kuna gharama nyengine wanazopaswa kulipia mbali na kununuwa mafuta ya magari yao:
"Saa zingine tunasukumwa bei hiyo kwa abiria......."
Mwenyekiti wa muungano huo eneo la Nyanza, Charles Obuya, anasema nauli itazidi kupanda kadri bei ya mafuta inavyoendelea kupanda. Ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumzia nyongeza ya asilimia hadi 20 ya nauli, uamuzi ulioafikiwa na Muungano wa Kitaifa wa Wamiliki wa Magari ya Uchukuzi unaoongozwa na Albert Karakacha. Anasema sekta ya uchukuzi imeathirika kwani idadi ya wanaosafiri imepunguwa.
"Tulipata mwongozo kutoka juu na tumeongeza kwa asilimia 20.........."
Mtaalamu maswala ya kiuchumi hapa Kisumu, Abel Barasa, ameiambia DW kuwa kauli ya serikali kudai haina uwezo wowote si ya kweli na amependekeza serikali ya Rais William Ruto kupunguza ushuru unaotozwa bidhaa za mafuta:
"Katika sekta ya Petroli serikali imeweka ushuru mwingi........"
Mdahalo wa kisiasa
Mdahalo kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta na gharama ya maisha kiujumla nchini Kenya ni swala ambalo linaendelea kuvutia hisia za serikali na wakati mwengine mgongano ndani yake.
Hivi karibuni Waziri wa Biashara Moses Kuria na msemaji wa rais kuhusu maswala ya kiuchumi, David Ndii, walikosolewa na Naibu Rais Rigathe Gachagua, aliyema kauli za wawili hao zilionekana kutojali hisia za Wakenya kwa uchumi wa taifa lao.