1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nyaraka zaonyesha Iran ilisaidia al Qaida

Elizabeth Shoo2 Novemba 2017

CIA imechapisha nyaraka zilizopatikana katika operesheni ya kumkamata kiongozi wa al Qaida, Osama bin Laden, mwaka 2011. Nyaraka hizo zimeibua maswali kuhusu Iran kuunga mkono kundi hilo la kigaidi.

https://p.dw.com/p/2muwK
Osama Bin Laden
Picha: picture-alliance/dpa

Maafisa wa kijasusi wa Marekani pamoja na waendesha mashtaka kwa muda mrefu wamekuwa wakisema kwamba Iran tangu mwaka 1991 imekuwa na uhusiano na kundi la al Qaida. Hiyo ni  moja ya taarifa zilizopatikana katika ripoti ya kurasa 19 iliyoandikwa kwa lugha ya Kiarabu na ambayo ni sehemu ya nyaraka 47,000 zilizochapishwa na CIA.

Iran kwa upande wake daima imekuwa ikikanusha uhusiano wowote na al Qaida. Hata hivyo, ripoti iliyochapishwa na CIA inaonyesha namna ambavyo bin Laden, aliyekuwa mtu mwenye itikadi kali za Kisunni na aliyetokea Saudi Arabia, nchi ambayo ni hasimu mkuu wa Iran, aliweza kuvuka mgawanyo wa kidini na kutafuta mshirika kwa Wairan wa Kishia, kwa lengo la kumlenga adui yao wa pamoja ambaye ni Marekani.

Ripoti inaeleza Iran iko tayari kumsaidia mtu yeyote anayetaka kuipiga Marekani. Shirika la habari la Marekani, AP, lilipatiwa nakala ya ripoti na nyaraka nyingine zilizokamatwa na CIA. Miongoni mwa mambo mengine, zinajumuisha pia video za harusi ya mtoto wa bin Laden, Hamza. Video hizo hazijawahi kuonyeshwa hadharani na ni mara ya kwanza kwa Hamza kuonekana akiwa mtu mzima. kabla ya hapo, picha na video zilizokuwa zimesambaa zilimwonyesha akiwa bado mtoto. Inaaminika kuwa Hamza bin Laden anaandaliwa kuwa kiongozi mpya wa al Qaida.

Iran yakanusha madai

Hamza bin Laden kwenye harusi yake
Hamza bin Laden kwenye harusi yakePicha: picture-alliance/CIA via dpa

CIA awali iliweka nyaraka za al Qaida mtandaoni lakini baadaye ikaziondoa, ikisema pamekuwa na hitilafu za kiufundi. Nyaraka hizo zinaelezea kile kinachoaminiwa kuwa historia ya uhisiano baina ya al Qaida na Iran. Inaonyesha kwamba Iran ilijitolea kuipa al Qaida fedha, silaha na kingine chochote ambacho kundi hilo lingehitaji. Iran pia ilikuwa tayari kuwapa magaidi mafunzo katika kambi za kundi la Hezbollah nchini Lebanon. Al Qaida kwa upande wake ilitakiwa kushambulia mali na miundombinu ya Wamarekani nchini Saudi Arabia.

Taarifa hiyo inaendana na ripoti ya serikali ya Marekani iliyoandikwa na kamisheni ya kupeleleza mashambulio ya kigaidi ya World Trade Center na Pentagon mwaka 2001. Ripoti hiyo inasema maafisa wa Iran walikutana na viongozi wa al Qaida nchini Sudan mwaka 1991 ama 1992. Kamisheni hiyo ileleza pia kuwa wanamgambo wa al Qaida baadaye pia walipatiwa mafunzo Lebanonon kutoka kwa kundi la wanamgambo wa Kishia, Hezbollah. Mpaka leo hii, Iran inaiunga mkono Hezbollah.

Hata hivyo, shirika la habari la Iran lisilo rasmi, Fars, leo limekanusha madai yote ya CIA, likisema huo ni mpango dhidi ya serikali ya Iran.

Mwandishi. Elizabeth Shoo/ap

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman