1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nyaraka za siri Libya - CIA / MI6 zilishirikiana na Gaddafi

4 Septemba 2011

Nyaraka za siri zilizogunduliwa baada ya waasi kuuteka mji wa Tripoli zimefichua kuwa mashirika ya ujasusi ya Marekani, Uingereza na mataifa mengine ya magharibi yalishirikiana na utawala wa Gaddafu

https://p.dw.com/p/12SiP
Waasi wa Libya wakishika doria katika mji mkuu TripoliPicha: dapd

Nyaraka za siri zilizogunduliwa baada ya waasi kuuteka mji wa Tripoli, zimefichua kuwa mashirika ya ujasusi ya Marekani, Uingereza na mataifa mengine ya magharibi yalifanya kazi kwa karibu na utawala wa Muammar Gaddafi uliondolewa madarakani. Nyaraka hizo zinaonyesha uhusiano mzuri na mawakala wa CIA na wa MI6 ya Uingereza. Walibadilishana taarifa na walishirikiana kukabidhiana watuhumiwa kwa ajili ya kuhojiwa na utawala ambao unafahamika kwa matumizi ya mateso.

Peter Bouckaert wa shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch, ambalo limesaidia kuzipata nyaraka hizo, limeyaita mahusiano hayo kati ya Marekani na utawala wa Gaddafi , kuwa ni ukurasa wa giza katika historia ya ujasusi nchini Marekani. Nyaraka hizo zinaonyesha kuwa CIA na MI6 ziliushauri utawala wa Gaddafi juu ya vipi inaweza kujitoa katika hadhi yake ya taifa linalosaidia ugaidi. Badala yake, mashirika yote mawili yalipokea taarifa za ujasusi kutoka Libya.