Nyakati nzuri na mbaya walizozipitia Vladimir Putin na Angela Merkel
Vladimir Putin amekuwa akiiongoza Urusi tangu 2000. Angela Merkel amekuwa akiiongoza Ujerumani tangu 2005. Uhusiano wa Rais huyo wa Urusi na Kansela wa Ujerumani umepitia misukosuko mingi. Ingawa mwanzo walianza vizuri.
Viongozi wanaoinukia
Mwaka 2002, Merkel alikuwa kiongozi wa kilichokuwa wakati huo chama cha upinzani cha Christian Democratic Union (CDU). Putin alikuwa wakati huo rais mpya wa Urusi. Baada ya kukutana na Putin nchini Urusi, Merkel aliwaambia wasaidizi wake kwa utani kwamba amefaulu "mtihani wa KGB" kwani aliweza kutuliziana macho na Putin.
Merkel kama Kansela mpya mtarajiwa
Putin alikuwa na urafiki na aliemtangulia Merkel, Gerhard Schröder, na viongozi hao wawili wameendeleza urafiki wao hadi hii leo. Mnamo 2005, ilikuwa wazi kwamba Merkel ndiye atakaempokonya kiti cha Ukansela Schröder wa Social Democrat. Hivyo Putin alikutana na Merkel katika ubalozi wa Urusi mjini Berlin.
Mwanamke anayejua kusikiliza kwa umakini
Takriban mwaka mmoja baadaye wakati Merkel ameshakuwa Kansela, Putin alisema: "Hatujuani vizuri sana, lakini nimevutiwa na uwezo wake wa kusikiliza," alimuambia mtangazaji wa kituo cha Ujerumani cha MDR kutoka Dresden, akiongeza kuwa uwezo wa kumsikiliza mwengine kwa umakini ni kitu nadra miongoni mwa wanasiasa wanawake.
Je, Putin alijaribu kumtisha Merkel kwa kutumia mbwa?
Sio siri kuwa Merkel anaogopa mbwa. Hata hivyo, Putin alimruhusu mbwa wake mweusi Konni kuranda kwenye eneo alikomkaribisha Kansela huyo mjini Sochi Januari 2007. Je, lengo lake lilikuwa ni kujaribu kumtisha? Hivyo ndivyo anavyodhani Merkel: "Naamini rais wa Urusi alikuwa anajua fika kuwa sikufurahia kuwa karibu na mbwa wake, lakini bado alimruhusu kuwa karibu nasi."
Merkel amrushia Putin maneno ya kejeli
Kufikia 2012, Vladimir Putin alikuwa ameanza kuwaminya waandishi wa habari na wapinzani wa kisiasa. Alipoulizwa juu ya uhuru wa vyombo vya habari wakati alipokuwa mjini Saint Petersburg, Merkel alijibu kwa nia ya kumkejeli kiongozi mwenzake: "Ikiwa nitakasirika kila wakati ninaposoma gazeti, basi nisingeweza kuwa Kansela hata kwa siku tatu," alisema Merkel.
Mazungumzo yaendelea uhusiano ukisuasua
Uhusiano kati ya Urusi na mataifa ya Ulaya ulizidi kuwa mbaya baada ya kulikamata kwa nguvu eneo la Crimea mwaka 2014. Lakini Putin aliviambia vyombo vya habari vya Ujerumani kwamba bado wanaendeleza uhusiano wao wa kikazi yeye na Kansela Merkel. "Namuamini. Ni mtu muwazi sana. Lakini kama binadamu mwengine, ana mapungufu yake," aliliambia gazeti la Bild la Ujerumani.
Sikusudii kumtukana lakini ...
Sikusudii kumtukana mtu yoyote, lakini matamshi ya Merkel yanatokana na hasira iliyojificha kwa muda mrefu kuhusu uhuru wenye kikomo," Putin aliviambia vyombo vya habari vya St. Petersburg 2017, akizungumzia matamshi ya Merkel wakati wa hotuba ya kampeni ya uchaguzi wakati akiwahimiza viongozi wa mataifa ya Ulaya kujitegemea wenyewe wakati wa mvutano na rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.
'Lazima tuwe tunazungumza'
Merkel alipowasili Sochi 2018, Putin alimkaribisha kwa kumpa shada la maua. Je, ni ishara ya kutafuta amani? Haijulikani. Lakini Merkel alisema mazungumzo kati yao lazima yaendelee. "Hata kama tunatofautiana sana katika baadhi ya maswala, lazima tuwe tunazungumza, vyenginevyo tutatumbukia kwenye ukimya wa milele."
Mkono wa 2020
Angela Merkel alikutana na Putin nchini Urusi Januari 2020. Tangu wakati huo uhusiano wao umeharibika tena kutokana na uingiliaji kati wa Urusi katika mzozo wa Ukraine, lakini pia jinsi taifa hilo linavyonyanyasa wapinzani, hasa Alexei Navalny aliyekamatwa baada ya kurudi Urusi kutoka Ujerumani alipokuwa akipatiwa matibabu.