1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nusu fainali Champions League kurindima

26 Aprili 2021

Wiki moja iliyopita, jamii ya kandanda iligubikwa na gumzo la Super League ya Ulaya ambapo timu 12 mahiri Ulaya zilikuwa zinapanga kujitenga na kucheza ligi ya kivyao ila mpango huo haukufika popote.

https://p.dw.com/p/3sb8T
Bildkombo | Paris Saint-Germain und Manchester City

Sasa baadhi ya timu hizo zinakutana wiki hii katika nusu fainali ya Champions League.

Jumanne, Chelsea watakuwa wanakwaana na Real Madrid halafu Jumatano, Manchester City watakuwa wanapambana na Paris Saint Germain.

Thomas Tuchel
Kocha wa Chelsea Thomas TuchelPicha: Andy Hoope/Solo Syndication/Daily Mail/picture alliance

Real Madrid watakuwa wametinga nusu fainali ya kwanza tangu 2018

Chelsea wameonyesha kuimarika pakubwa tangu kuachishwa kazi Frank Lampard na Thomas Tuchel kuchukua mikoba huku kocha huyo raia wa Ujerumani, akipania kufuzu kwenye fainali yake ya pili mfululizo kwenye Champions League baada ya kulazwa na Bayern Munich katika fainali ya msimu uliopita.

Madrid nao watakuwa wametinga nusu fainali yao ya kwanza tangu mwaka 2018 na kwenye La Liga ya Uhispania, wanafanya vizuri ingawa wako kwenye shinikizo kutoka kwa Atletico Madrid na Barcelona.

Huku ikiwa Madrid wamelishinda kombe hilo mara kumi na tatu na Chelsea wakiwa waliebuka na ubingwa mwaka 2012, Manchester City na PSG wao wanataka kuonja ladha ya ubingwa kwa mara ya kwanza.

Itakumbukwa kwamba City waliwafunga PSG mwaka 2016 na kufuzu kwenye nusu fainali yao ya kwanza kabisa ila PSG wamepata motisha zaidi msimu huu kwa kuwa wao ndio waliowabandua mabingwa watetezi Bayern Munich.