NRM yatimiza miaka 30 madarakani
26 Januari 2016Wakati vuguvugu la NRM lilipoingia madarakani mwaka 1986, Rais Yoweri Museveni alifanya juhudi kuleta pamoja makundi mbalimbali ya waasi na kubuni serikali ya umoja wa kitaifa. Miongoni mwao ni naibu waziri mkuu wa tatu, Jenerali Moses Ali, aliyekuwa akiongoza kundi la waasi walioendesha harakati zao kaskazini magharibi mwa Uganda.
Haya yamekuwa mafanikio makubwa, anasema mchambuzi wa masuala ya kisiasa Akol Amazima, "kwani utawala umekuwa thabiti na kuwezesha wananchi kuondokana na maisha ya mashaka."
Katika kipindi hiki cha miaka 30, Rais Museveni ameongoza serikali ambayo imetoa fursa nyingi kwa Waganda na pia wageni mkiwemo wakimbizi kuishi na kutangama ipasavyo.
Mariam Kabosi, mkaazi wa Mtaa wa Ntinda jijini Kampala, anasema utawala wa NRM "umewawezesha wanawake kushiriki katika ngazi mbalimbali za uongozi kutokana na fursa za elimu na usawa wa kijinsia."
Uchaguzi, katiba na Museveni
Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu, ambao kwa mara nyengine unamshuhudia Museveni akiwania muhula mwengine madarakani. Uchaguzi wa kwanza ulifanyika mwaka 1996 chini ya katika mpya ya mwaka 1995 iliyoelezea kuwa rais angetawala kwa awamu mbili.
Lakini baadaye Museveni aliivunja ahadi yake ya kutotawala muda mrefu na kubadili katiba. Wakosoaji wake wanasema hilo limeufanya umaarufu wake umezidi kuporomoka mwaka hadi mwaka. Hata waliokuwa wafuasi wake wameshuhudiwa wakimpinga waziwazi na kujiunga na upinzani, akiwemo Amama Mbabazi, katibu mkuu wa zamani wa NRM na waziri mkuu wa Museveni.
Juu ya yote, utawala wa miaka 30 wa Museveni na NRM umewezesha ukuaji wa uchumi kwa kasi kubwa nchini Uganda hasa kutokana na sera za biashara huru na kustawisha mazingira bora kwa wawekezaji. Aidha ujenzi na upanuzi wa miundo mbinu kama vile barabara na kusambaza nishati ya umeme, hatua ambazo zimewezesha kuwepo kwa tabaka la kati kiuchumi ambalo linajumuisha pia watu wasio na elimu ya juu.
Mwandishi: Lubega Emmanuel/DW Kampala
Mhariri: Iddi Ssessanga