Norway, Ireland, Uhispania kutambua taifa la Palestina
23 Mei 2024Norway, Ireland na Uhispania zimetangaza jana Jumatano kwamba zitalitambua taifa la Palestina, katika hatua ya kihistoria lakini ya kiishara inayozidisha kutengwa kwa Israel, zaidi ya miezi saba tangu ianzishe vita dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Israel imelaani uamuzi huo na kuwaita nyumbani mabalozi wake katika mataifa hayo matatu.
Maafisa wa Palestinawamepongeza matangazo hayo na kuyataja kama uthibitisho wa shauku yao ya miongo kadhaa ya kuunda taifa lao katika eneo la Jerusalem Mashariki, Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza, maeneo ambayo Israel iliyanyakua katika Vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka 1967 na inaendelea kuyadhibiti.
Soma pia: Ireland, Uhispania, Norway zatangaza kuitambua Palestina kma taifa huru
Wakati mataifa takribani 140, ambayo ni zaidi ya theluthi mbili ya Umoja wa Mataifa, yanalitambua taifa la Palestina, mtirirko wa matamko ya Jumatano unaweza kuongeza kasi katika wakati ambapo hata washirika wa karibu wa Israel wameongeza ukosoaji kutokana na inavyoendesha vita vyake Gaza.