1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

Njinga Mbande - Shujaa wa kidiplomasia

8 Februari 2018

Njinga Mbande alikuwa mwanadiplomasia na mkuu wa jeshi wa karne ya 17, na alitumia mbinu zake zote kupambana na utawala wa kikoloni wa Ureno. Anachukuliwa kama mwanamke shupavu zaidi katika kupinga ukoloni.

https://p.dw.com/p/2qDMg
African Roots Njinga Mbande
Picha: Comic Republic

Njinga Mbande - Shujaa wa kidiplomasia

Anajulikana kwa: Njinga Mbande anajulikana kwa kupambana na utawala wa kikoloni wa Kireno katika maisha yake yote kwa kutumia mbinu za kidiplomasia na kijeshi katika eneo ambalo leo hii ni Angola.

Ameshutumiwa kwa: Ameshutumiwa kwa kuwa katili kwa kumuua mpwa wake ili apate uongozi wa Ndongo, anashutumiwa kwa kuunga mkono utumwa katika eneo lake, kwani aliingia kwenya mkataba na Wareno ili wapate watumwa pamoja na Wadachi.

Njinga asiye na maana: Mwaka wa 1622, Ngola Mbande aliyekuwa anatawala na ambaye alikuwa ni kaka yake Njinga alimtuma aende Luanda kujadili kuhusiana na masuala ya mkataba wa usalama wa eneo hilo la Ndongo na gavana Mreno aliyekuwa huko. Alipewa tambara badala ya kiti cha kuketia, jambo lililomaanisha kwamba alichukuliwa kama mtu asiye na maana. Njinga alimuamrisha mmoja wa watumishi wake kupiga magoti na awe kama kiti chake. Na baada ya hapo aliendelea na mazungumzo hayo.

African Roots Njinga Mbande
Njinga Mbande akiwa akiwa amemkalia mtumishi wakePicha: Comic Republic

Njinga aliyeelimika: Alikuwa anaweza kuzungumza lugha tofauti tofauti za nchini humo pamoja na Kireno. Pia alikuwa anajua kusoma na kuandika kwani alikuwa akiandika barua zake mwenyewe za majadiliano ya uhuru na wakoloni, na jambo hili lilichangiwa kutangamana kwake na wamishonari na Wareno. Alikuwa pia na ujuzi wa masuala ya kidplomasia na kijeshi mambo ambayo yalimsaidia alipokuwa akizungumza na Wareno na Wadachi.

Njinga mpiganaji: Njinga alitambulishwa katika mapigano kwa niaba ya babake, mfalme Kiluanji. Katika uongozi wake, alipigana kama mwanajeshi mbele ya jeshi lake kama thibitisho la ukakamavu wake. Kulingana na wanahistoria, Njinga alikataa kupewa jina la Malkia na badala yake alijichukulia kama mfalme, na alikuwa kama mwanamume katika jamii.

 

Carla Fernandes na Gwendolin Hilse wamechangia kuandika makala hii. Ni sehemu ya makala maalum za  mfululizo wa "Asili ya Afrika", ushirikiano kati ya shirika la DW na taasisi ya Gerda Henkel.

 

Tafsiri: Jacob Safari/Africa Roots

Mhariri: Gakuba Daniel