1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nini kitatokea baada ya kifo cha Zenawi?

22 Agosti 2012

Baada ya Ethiopia kumpoteza kiongozi wake mwenye nguvu sana, suali linaloulizwa ni nini kitatokea baada ya kifo cha Waziri Mkuu Meles Zenawi, hasa inapozingatiwa mjengeko wa taifa hilo lenye makabila mengi.

https://p.dw.com/p/15u1B
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Haile Mariam Desalegne.
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Haile Mariam Desalegne.Picha: CC-BY-SA- World Economic Forum

"Waziri Mkuu atakuwa tayari ameshapona kufikia maadhimisho wa mwaka mpya wa Ethiopia hapo Septemba 11", ndivyo msemaji wa serikali, Bereket Simon, alivyokuwa amewaambia waandishi wa habari na mabalozi hivi karibuni, walipoulizia kuhusu afya ya Meles Zenawi.

Lakini hakuna aliyetaka kumuamini. Tayari kukosekana kwa kiongozi huyo machachari kwenye mkutano wa kilele wa mataifa ya Afrika hapo mwezi Julai mjini Addis Ababa kulishazua shaka zisizoweza kuzimwa kirahisi. Kiongozi huyo, ambaye nchini Ethiopia hutambuliwa zaidi kwa jina lake la kwanza la Meles, asingeweza kabisa kukosa mkutano huo lau angelikuwa na afya nzuri.

Jumanne asubuhi, waziri wa habari Bereket Simon akakutana tena na waandishi wa habari mjini Addis Ababa kwa kuthibitisha kifo cha Meles Zenawi. Wakati huo huo, televisheni ya taifa ikaripoti mkutano huo kama ulivyo. Nyuma ya hapo, gazeti moja lililowahi kuvumisha kuzorota kwa afya ya Zenawi lilifungiwa na serikali.

Ethiopia, serikali ina nguvu sana

“Tusisahau kwamba Ethiopia ina taasisi imara sana za dola. Kwa hivyo, si kwamba kwa kifo cha waziri mkuu, mara moja kila kitu kitaporomoka. Bila ya shaka itachukuwa muda kuonesha nani mwenye udhibiti wa taasisi hizo, lakini hilo si suala la kuliamulia kwa muda mchache.” Anasema Sally Healy wa Taasisi ya Bonde la Ufa iliyopo London.

Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia, Marehemu Meles Zenawi.
Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia, Marehemu Meles Zenawi.Picha: AP

Kikatiba, naibu waziri mkuu ndiye anayechukuwa majukumu ya waziri mkuu pindi hali kama hii ikitokea. Kwa sasa nafasi hiyo inashikiliwa na waziri wa mambo ya nje, Hailemariam Desalegne. Mhandisi huyo wa maji na mshauri wa zamani wa Meles, Hailemariam anachukuliwa kama msomi mtiifu, lakini asiye na uthubutu wa shujaa wake, Meles.

Hailemariam si wa kabila la Tigre analotoka Zenawi, wala si muumini wa madhehebu ya Orthodox aliyofuata Zenawi. Mgombea mwenye kuitaka nafasi ya Meles, kwa hivyo lazima akabiliane na makada wa chama cha Ukombozi cha Tigraya, TPLF, na pia jeshi lenye nguvu kubwa.

Vile vile baraka za kanisa la Orthodox ni muhimu sana kwa kiongozi mkuu huyo wa kwanza nchini Ethiopia kutokea madhehebu ya Kiprotestanti. Ingawa kabila lake la Wolayta ni kubwa sana, lina uwakilishi mdogo sana. Hata nafasi ya uraisi waliyopewa ni ya kiheshima zaidi na sio ya kiutendaji.

Mapambano ya madaraka yaanza

Vyanzo vya kuaminika vya Waethiopia wanaoishi nje, vinasema kwamba tayari kuna mapambano ya kupigania madaraka ndani ya tabaka tawala na katika wagombea wenye nafasi kubwa zaidi, Hailemariam si miongoni mwao.

Marehemu Meles Zenawi na mkewe, Azeb Mesfin.
Marehemu Meles Zenawi na mkewe, Azeb Mesfin.Picha: dapd

Wanaotajwa ni pamoja waziri wa afya na msiri mkubwa wa Meles, Tewodros Adhanom na mwanadiplomasia wa TPLF na mtu mwengine wa karibu na Meles, Berhane Gebre Kristos. Pia mjane wa Meles, mfanyabiashara Azeb Mesfin, anatajwa. Azeb ni mjumbe wa kamati kuu ya watu tisa yenye nguvu kubwa kisiasa katika chama tawala na amejikusanyia utajiri mkubwa, ambao mara kadhaa huhusishwa na ufisadi.


Jakkie Cilliers, mkurugenzi wa Taasisi ya Masomo ya Usalama ya Afrika Kusini, ISS, anasema si rahisi kulijaza ombwe la kiuongozi nchini Ethiopia.

“Bila ya shaka, hiki ni kipindi hatari sana, ambacho kinaweza kusababisha ukosefu wa utulivu. Lakini nafikiria chama tawala kimejitayarisha kwa hali hii ndani ya wiki chache zilizopita na natarajia tutashuhudia kipindi cha mpito cha haraka na kilichoratibiwa vyema. Lakini ubadilishanaji wa madaraka kwa njia kama Ethiopia, ambako nguvu za serikali zilikuwa za mtu binafsi, daima ni jambo gumu.” Anasema Cilliers.

Kwa vyovyote vile, kifo cha Meles Zenawi kitafunua mengi yaliyokuwa yamefunikika kwa zaidi ya miongo miwili ya utawala wake, si ndani tu, bali hata nje ya nchi hiyo ya mashariki ya Afrika. Kwa mfano, suala la wanajeshi wa Ethiopia walioko Somalia kupigana na al-Shabaab, makubaliano yenye utata na Misri juu ya haki za kutumia maji ya Mto Nile na uhasama kati ya Ethiopia na Eritrea.

Mwandishi: Ludger Schadomsky/Mohammed Khelef/DW
Mhariri: Othman Miraji