Nini kitafuata baada ya kusitishwa mapigano Gaza?
21 Januari 2009Milio ya mabomu, maroketi na mizinga pamoja na risasi angalau haisikiki sasa katika Ukanda wa Gaza tangu jumapili iliopita baada ya Israel kutangaza kwamba inasitisha mapigano yaliodumu siku 22 , na chama cha Wapalastina cha Hamas nacho kufuata vivyo hivyo muda mfupi baadae. Lakini usitishaji huu wa mapigano ni wenye kulegalega, Israel ikishikilia kwamba ina haki ya kushambulia ikiwa majeshi yake yatashambuliwa, ikiwa maroketi ya Wapalastina hayatakoma kuishambulia miji ya Israel, na ikiwa Chama cha Hamas kitajipatia silaha kwa njia ya magendo, kama kilivokuwa kikifanya hapo kabla, kupitia mpaka wa Rafah pamoja na Misri. Chama cha Hamas kimeipa Israel wiki moja iondoshe kabisa majeshi yake kutoka ardhi ya Gaza, Israel iwache kuuzingira ukanda huo na mipaka ya Gaza iwe wazi kwa bidhaa kutoka nje kuingia na kutoka.
Tangu kuanza mashambulio ya Israel katika Ukanda wa Gaza hapo Disemba 27, zaidi ya Wapalastina 1,300 wameuwawa, wakiwemo watoto na wanawake, na zaidi ya 5,300 wamejeruhiwa. Peke yake, siku ya jumapili, muda mfupi baada ya usitishaji mapigano kuanza kufanya kazi, ziligunduliwa maiti 95 chini ya vifusi vya majumba yalioanguka kutokana na mashambulio ya Israel kutoka angani, baharini na nchi kavu. Kwa upande wa Israel, wanajeshi wake kumi waliuwawa na pia raia watatu kutokana na mashambulio ya maroketi. Kwa makisio ya Wapalastina, karibu asilimia 14 ya nyumba zote katika Ukanda wa Gaza zimebomolewa au kuharibiwa, umeme na usambazaji wa maji unakosekana kwa sehemu kubwa, na misikiti 20 imegeuka kuwa madongo tu.
Waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, alisema hivi muda mfupi kabla ya kuanza kutekelezwa usitishaji mapigano:
"Malengo tuliojiwekea kabla ya kuanzisha operesheni yamefikiwa kikamilifu, na zaidi ya hapo. Chama cha Hamas kimepata pigo kubwa, kijeshi na katika uongozi wake."
Licha ya hayo alisema Israel imepata ahadi kutoka Marekani na nchi nyingine za Magharibi kwamba kutakomeshwa mtindo wa Hamas kujipatia silaha kutoka ngambo na hasa usafirishaji wa silaha hizo kwa magendo na kupitia mahandaki ya chini ya ardhi katika mpaka wa Rafah baina ya Misri na Gaza.
Naye Osama Hamdan, msemaji wa chama cha Hamas huko Lebanon alimjibu Ehud Olmert papo hapo, kwa kusema:
"Ikiwa Israel haitaondosha majeshi yake kutoka Ukanda wa Gaza, basi upinzani dhidi ya Israel utasonga mbele, hamna mtu atakayeweza kuuzuwia, na jambo hilo litambuliwe na Olmert."
Inasemakana mbinyo wa kimataifa kutaka Israel isitishe mashambulio yake, na baadae majeshi yake yaondoke Gaza ulikuwa mkubwa mno, licha ya kwamba serekali ya nchi hiyo ilidai ilifanya hivyo kuzuwia mashambulio ya maroketi yanayofyetuliwa kutokea Gaza kwendea katika miji ya Israel.
Maroketi ya Israel kuangukia katika majengo na shule za Umoja wa Mataifa huko Gaza ambako watu walikimbilia kutafuta hifadhi ni mambo ambayo jamii ya kimataifa yalikuwa hayawezi kuyastahamilia zaidi.
Haikataliki kwamba usitishaji huu wa mapigano umechangiwa sana na juhudi za kidiplomasia za Misri za kupatanisha baina ya Israel na Wapalastina.
Ili kuikabili hali hii mpya, Rais Husni Mbarak akaitisha mkutano wa haraka huko Sharm al-Sheikh, Misri, na kuwaalika rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy; Kansela Angela Merkel wa Ujerumasni; waziri mkuu wa Uengereza, Gordon Brown; waziri mkuu wa Spain, Jose Luis Zapatero; waziri mkuu wa Jamhuri ya Cheki, Mirek Topolanek, na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon. Pia alikuweko Mfalme Abdullah wa Jordan. Madhumuni ni kuudumisha usitishaji wa mapigano katika Gaza, namna takwa la Israel la kukomeshwa kupitishwa silaha za Hamas katika mpaka wa Rafah, kufunguliwa mipaka na Gaza, kuleta umoja wa Wapalastina baina ya serekali ya Mahmud Abbas huko Ramallah na utawala wa Hamas huko Gaza, kuijenga upya Gaza na mwishowe kuufua tena mwenendo wa amani baina ya Israel na Wapalastina ili kufikia lile lengo la kuwa na dola mbili, Israel na Palastina, zikiishi ubavu kwa ubavu.
Katika mkutano huo Kansela Angela Merkel wa Ujerumani aliweka wazi kwa kusema:
"Sote tunahisi kwamba lazima ihakikishwe kusafirishwa silaha kwa magendo, kwa njia ya bahari au nchi kavu, kunakomeshwa, na kile ambacho tunachoweza kutoa, katika msaada wa kiufundi kwa ajili ya jambo hilo, tutachangia."
Waziri mkuu wa Uengereza, Gordon Brown alisema huko kwamba ni jukumu la nchi za Ulaya kuziendeleza juhudi za Rais Husni Mubarak wa Misri kupata amani ya kudumu:
"Naamini kwamba kwa vile sasa Rais Obama anaingia madarakani na kazini, ni jukumu letu sisi nchi za Ulaya zinazowakilishwa hapa- Italy, Spain, Ujerumani, Cheki na Rais wa Ufaransa- sote sisi hapa tujenge juu ya kile kilichoundwa na Rais Husni Mubarak na kusonga mbele kwa haraka kuelekea suluhisho la amani ya kudumu ambalo litaitambua Israel ilio katika salama na nchi ya Palastina itakayoweza kufanya kazi na kuungwa mkono na nchi 57 ambazo zimesema zitaitambua."
Kama usitishaji huu wa mapigano utasimama, kazi itakayofuata itakuwa kuijenga upya Gaza, ambapo fedha nyingi zitahitajika. Nchi za Kiarabu katika mkutano wao wa kilele huko Doha zimetoa ahadi ya kufanya hivyo, na pia nchi za Ulaya huko Sharm al-Sheikh. Japokuwa nchi za Umoja wa Ulaya zimesema zitafanya hivyo, lakini kamishina wa mambo ya kigeni wa umoja huo, Benita Ferrero-Waldner, amesema majengo na miundo mbinu haitajengwa upya ikiwa Chama cha Hamas kitabakia madarakani katika eneo hilo. Umoja wa Ulaya unakiona Chama cha Hamas kuwa ni cha kigaidi na unakataa kufanya shughuli nacho. Bibi Ferrero-Waldner alishauri kwamba msaada wa kimataifa kuijenga Gaza utatolewa ikiwa Chama cha Fatah cha Rais wa Wapalastina, Mahmud Abbas, ambacho kina siasa za wastani, kitarejea katika eneo hilo. Hamas kilikamata mamlaka huko Gaza Juni mwaka 2007, na mazungumzo ya kuyapatanisha makundi hayo mawili hadi sasa hayajafanikiwa.
Viongozi wa Ulaya walisema wazi kwamba wanaunga mkono haki ya Israel kujilinda ndani ya mipaka yake, lakini, wakati huo huo, Israel pia ilitakiwa isonge mbele na mwenendo wa amani pamoja utawala wa Wapalastina wa Rais Mahmud Abbas ili iamuliwe hali ya baadae ya mipaka katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na suala la kuwa na dola mbili.
Vita vya Gaza pia tusidharau kwamba vimewagawa zaidi Waarabu. Pengo limezidi baina ya watawala wa Kiarabu walionyamaa kimya huku Israel ikiishambulia vikali Gaza na wananchi waliokwenda mabarabarani kuupinga uvamizi huo. Zaidi, sura ilijitokeza kwamba Wapalastina wenyewe kwa wenyewe hawana msimamo mmoja katika suala la namna ya kuzikomboa ardhi zao. Matokeo ni kwamba Mahmud Abbas amepoteza heba yake mbele ya wananchi wake, anaonekana anajitenga zaidi na zaidi na malengo ya kuendesha mapambano ya kisilaha. Cha kusikitisha zaidi ni kwamba hata kama anajifanya kuwa mshirika wa kuaminika katika mazungumzo na Israel, hadi sasa Israel haijampa chochote kwa yeye kujivunia mbele ya Wapalastina wenzake.
Kwa hivyo, licha ya risasi na mizinga kutulia huko Gaza, amani iko mbali, mbali zaidi kuliko pale yalipoanza mapigano hapo Disemba 27. Tujiulize: Naye waziri mkuu wa Israel alikuwa na haya ya kusema kuwapoza Wapalastina wa Gaza:
" Nataka kuomba radhi kwa niaba ya serekaliy a Israel kwa kila mtu ambaye sio kwa njia ya haki aliathirika huko Gaza kutokana na operesheni hii."
Sijui limepokelewa vipi ombi hilo kwa jamaa wa watu waliokufa, kwa waliojeruhiwa, na kwa watu waliopoteza mali zao na kujihisi hawana hatia yeyote na vita hivi.