Nigeria,Jamhuri ya Afrika Kati na Pistorius magazetini
16 Mei 2014Tunaanzia Nigeria na kisa cha kuhuzunisha cha kutekwa nyara watoto zaidi ya 200 wakike walipokuwa shule katika eneo la kaskazini mashariki ya Nigeria.Wanamgambo wa itikadi kali ya dini ya kiislam Boko Haram ndio waliowateka nyara wasichana hao,na wanadhamiria kuwauza kama watumwa.Gazeti la Die Zeit linaelezea jinsi magaidi hao wanavyozidi kueneza vitisho nchini Nigeria huku serikali ikishindwa kufanya chochote licha ya msaada kutoka nchi za magharibi.Die Zeit linajiuliza nini kitatokea hivi sasa,ndo kusema serikali itajadiliana na magaidi?Boko Haram wameonyesha kanda ya video ya wasichana hao waliovalishwa mabui bui wakishurutisha kuwaachia huru wasichana hao ikiwa wafuasi wao nao wataachiwa huru na serikali.Die Zeit linazungumzia maandamano yanayoendelea katika kila pembe ya nchi hiyo kulalamika dhidi ya uzembe wa serikali.Upande wa upinzani nchini Nigeria unamlaumu rais Goodluck Jonathan kuufumbia macho makusudi uasi katika eneo la kaskazini mashariki ambalo ni ngome ya Boko Haram,linaandika die Zeit linalojiuliza,opereshini ya kuwakomboa wanafunzi hao wa kike inawezekana bila ya kusababisha mauwaji ya jumla jamala?Die Zeit linamaliza kwa kumnukuu mmojawapo wa wanachama wa baraza la wazee wenye busara Pogu Petrus akisema serikali haina njia nyengine isipokuwa kujadiliana na Boko Haram tu?
Msiba wa kutekwa nyara wasichana zaidi ya mia 200 na Boko Haram umegonga pia vichwa vya habari vya majarida mfano wa der Stern linalozungumzia juu ya wazee kukata tamaa na serikali kuzidiwa.
Kiu cha kujua ukweli chamwangamizia maisha
Katika jamhuri ya Afrika kati matumizi ya nguvu na mauwaji hayana kikomo.Watu wanatiwa moto wahai.Waandishi habari wanauliwa.Gazeti la Frankfurter Allgemeine limeandika kuhusu kisa cha kuuliwa ripota wa kifaransa Camille Lepage."Alikuwa anatafuta ukweli wa mambo" ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya Frankfurter Allgemeine linalomtaja ripota huyo kuwa mwandishi habari asiyehofia hatari-muhimu kwake ni kupiga picha na kuzungumzia mauwaji yanayotokea.Picha zake zimefika katika kila pembe ya dunia kupitia magazeti ya Guardian la Uingereza,Le Monde la Ufaransa,Washington Post,la Marekani,mpaka kufikia jarida la der Spiegel la Ujerumani.Camille Lepage alikuwa akiripoti pia kuhusu Sudan Kusini alikokuwa akiishi tangu julai mwaka 2012.Walikuwa wanajeshi wa Ufaransa waliogundua maiti yake wiki hii katika eneo la magharibi la jamhuri ya Afrika kati.Alikuwa njiani kuelekea Amada Gaza ambako ripoti zinasema waasi wa Seleka waliwauwa wakristo wasiopungua 150 wiki mbili zilizopita."Kiu chake cha kutafuta habari na kuujua ukweli wa mambo ndicho kilichomwangamizia maisha yake" linamaliza kuandika gazeti la Frankfurter Allgemeine.
Pistorius atakiwa ende hospitali ya wagonjwa wa akili
Mada yetu ya mwisho katika ukurasa huu wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii inahusu uamuzi wa hakimu mmoja wa Afrika kusini anaeongoza kesi dhidi ya Oscar Pistorius,aliyeamuru mwanariadha huyo mlemavu apelekwe katika hospitali ya wagonjwa wa akili kuangalia kama akili yake inafanya kazi sawa sawa au la."Kuna uwezekano kwamba mshitakiwa ana upungufu wa akili"limeandika Frankfurter Allgemeine lililomnukuu jaji Thokozile Masipe akisema.Frankfurter Allgemeine linahisi uamuzi huo unaweza kuharakisha kumalizika kesi hiyo.Pindi uchunguzi ukibainisha Pistorius ana upungufu wa akili,atalazimika kupelekwa katika kituo cha serikali cha matibabu ya wagongjwa wa akili na kusalia katika kituo hicho pengine hadi mwisho wa maisha yake.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman