1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria yamtimua Stephen Keshi

17 Oktoba 2014

Mabingwa watetezi Nigeria wameonekana kuyumbayumba katika safari ya kutetea kombe hilo, na ndio maana wakaamua kumtimua kocha Stephen Keshi. Nafasi yake imechukuliwa kwa muda na Shaibu Amodu

https://p.dw.com/p/1DXv1
Nigeria Fußball Nationalmannschaft Trainer Stephen Keshi
Picha: Phil Walter/Getty Images

Mashabiki wa kandanda Nigeria wameelezea hisia tofauti kuhusiana na hatua hiyo ambalo ilitangazwa hata baada ya Super Eagles kuizaba Suda magoli matatu kwa moja siku moja kabla, matokeo ambayo yaliirejesha katika mkondo sahihi kampeni yao ya kufuzu baada ya kushindwa mechi mbili na kutoka sare moja.

Keshi, ambaye ni nahodha wa zamani wa timu ya taifa, aliiongoza Nigeria kushinda ubingwa wa Afrika mwaka wa 2013 nchini Afrika Kusini na pia akaipeleka nchi yake katika Kombe la Dunia nchini Brazil mwaka huu, ambako walifika katika duru ya pili kabla ya kubanduliwa nje na Ufaransa.

ERNEST OBEM ni mkaazi wa Abuja. na anasema "maoni yangu ni kuwa hangefutwa kazi kwa sababu aliiongoza timu kwa ushindi mkubwa. Keshi amefanya vyema katika timu. Hakuna asiyekosea. Naamini hata kama wana mtu wanayemtaka kama kocha wa kigeni, wangebaki na Keshi hadi uamuzi huo utakapofanywa".

Fußballtrainer WM 2010 Shaibu Amodu Nigeria Flash-Galerie
Shaibu Amodu amechaguliwa kushika usukani kwa mudaPicha: AP

BEATRICE OKOTIE ni mfanyakazi mstaafu wa umma: "Sisi wanageria tuna furaha kuwa Stephen Keshi amefutwa kazi kwa sabbau tunataka kiwango cha michezo Nigeria kiimarike. Tunapozungumza kuhusu michezo, ni mpango unaoleta furaha kwetu. Tunajua kuwa baadhi ya wanasiasa wametukasirisha lakini tukizungumza kuhusu michezo, na hasa kandanda nchini Nigeria tunafurahia.

SIMON MARSHAL ni mfanyabiashara: "Mwingine amesema "Naam, nadhani Stephen Keshi kufutwa kazi ni hatua nzuri katika mkondo unaofaa. Wakati mtu anapoishiwa mawazo yake na hajiwezi tena kufanya vyema, ni vyema umtafute mwingine ambayo unajua anaweza kupambana na changamoto hizo na kuzitatua".

Nafasi ya Keshi imechukuliwa na muungano wa makocha unaoongozwa na Shaibu Amodu, ili kushughulikia mechi mbili za mwisho za kufuzu katika dimba la AFCON zitakazochezwa mwezi Novemba.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri:Yusuf Saumu