1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria yaipita Afrika Kusini kiuchumi

7 Aprili 2014

Nigeria imekuwa taifa kubwa zaidi kiuchumi barani Afrika, na kuipiku Afrika Kusini, baada ya takwimu mpya kupandisha pato la jumla la ndani la taifa hilo hadi kufikia dola za marekani zaidi ya bilioni 500

https://p.dw.com/p/1Bd1h
Picha: Getty Images

Wakala wa takwimu wa Nigeria ulitangaza pato jipya la taifa hilo linaloongoza kwa uzalishaji mafuta barani Afrika kuwa ni dola za Marekani bilioni 509.9, karibu mara mbili ya kiwango kilichokuwa kinakadiriwa kabla ya kukokotolewa upya. Thamani hii mpya ya pato la ndani la Nigeria inajumlisha sekta kama vile mawasiliano, habari na teknolojia, muziki, biashara za mtandaoni na fillamu za Nollywood, ambazo hazikuwepo wakati mahesabu ya mwisho yalipofanyika mwaka 1990.

Licha ya mafanikio ya kiuchumi, Nigeria bado inakabiliwa na changamoto kubwa zikiwemo miundombinu duni.
Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan.Picha: picture-alliance/AP Photo

Wakati huo kulikuwepo na simu za mezani 300,000. Hivi sasa Nigeria ina watumiaji wa simu za mkononi milioni 100. Takwimu hizo mpya zinazingatia ukuaji katika sekta za kilimo na utalii, ambazo zimekuwa kwa kiasi kikubwa tangu nchi hiyo iliporejea kwenye mkondo wa demokrasia mwaka 1999, na kukomesha miongozo kadhaa ya utawala wa kidikiteta.

Afrika Kusini yaachwa mbali

Nigeria sasa imeipiku Afrika Kusini ambayo pato lake la jumla la ndani la dola za Marekani bilioni 353 ndiyo lilikuwa linahesabiwa kuwa kubwa zaidi barani, na ambayo ndiyo nchi pekee ya Kiafrika mwanachama wa kundi la mataifa 20 yaliyoendelea kiuchumi G20.

Meneja wa uwekezaji Kevin Daly kutoka shirika la usimamizi wa mali la Aberdeen la nchini Uingereza, na ambalo linawekeza Nigeria, alisema mafanikio ya Nigeria ni ukumbusho kuwa Afrika inasonga mbele licha ya changamoto inazokabiliana nazo kwa sasa. Daly alibainisha kuwa ni bilionea wa Kinigeria Aliko Dangote, ambaye anajenga kiwanda kikubwa zaidi binfasi cha kusafisha mafuta barani Afrika.

Wawekezaji watavutiwa na ukweli kwamba, wakati mafuta yanaendelea kuwa chanzo kikuu cha mapato ya serikali, kwa asilimia 80, uzalishaji wa mafuta unapungua wakati sekta za kilimo na huduma za mawasiliano zinazidi kushamiri.

Nigeria imekuwa mpokeaji mkubwa zaidi wa uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni barani Afrika licha ya matatizo mengi yanayoikabili, kuanzia rushwa iliyokithiri na wizi wa mafuta vinavyoigharimu nchi karibu dola milioni 20 kila siku, hadi kwenye uasi wa kundi la Kiislamu kaskazini-mashariki, ambao umewaua watu zaidi ya 1,200 mwaka huu peke yake, na umeme usiyo wa uhakika, unaozifanya biashara zitegemee majenereta.

Licha ya mafanikio ya kiuchumi, Nigeria bado inakabiliwa na changamoto kubwa zikiwemo miundombinu duni.
Licha ya mafanikio ya kiuchumi, Nigeria bado inakabiliwa na changamoto kubwa zikiwemo miundombinu duni.Picha: Pius Utomi Ekpei/AFP/Getty Images

Waziri wa fedha Ngozi Ikonjo-Iweala aliuwambia mkutano wa waandishi wa habari jana kuwa takwimu hizo mpya zinaifanya Nigeria kuwa nchi ya 26 kwa uchumi mkubwa duniani, na zinapandisha pato lake la mtu mmoja mmoja hadi kufikia dola za Marekani 2,688, na kushika nafasi ya 121 duniani kutoka 135.

Maskini hawanufaiki

Hata hivyo kiwango hicho bado ni kidogo ikilinganishwa na Afrika kusini ambayo pato lake la mtu mmoja mmoja ni dola za Marekani 7,336 kwa wakaazi wake milioni 48. Mchambuzi wa masuala ya fedha Bismark Rewane aliyaita marekebisho hayo kuwa ni majivuno tu, na kwamba maisha ya raia hayataboreka kesho kwa sababu ya tangazo hilo.

Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira nchini Nigeria kilipanda kutoka asilimia 12.7 mwaka 2007 hadi asilimia 23.9 mwaka 2011, wakati benki ya dunia ikisema ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana ni asilimia 38, lakini wachambuzi wanasema kinakaribia asilimia 80 katika maeneo mengi ya nchi.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/ape,rtre,afpe
Mhariri: Hamidou Oummilkheir.