1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria na Senegal zatinga Nusu Fainali ya AFCON

Admin.WagnerD11 Julai 2019

Nigeria na Senegal zimefanikiwa kupenya na kuingia hatua ya nusu fainali ya michuano ya kandanda ya mataifa ya Afrika AFCON inayoendelea kutimua vumbi nchini Misri.

https://p.dw.com/p/3Lesv
Africa Cup of Nations 2019 - Viertelfinale - Senegal gegen Benin
Picha: Reuters/M. A. El Ghany

Katika michezo miwili ya robo fainali iliyochezwa jana Jumatano Nigeria iliiadhibu Afrika ya Kusini bao 2 kwa 1 huku goli la ushindi likiwekwa wavuni kutoka mpira wa kona uliochongwa vizuri na William Ekong, dakika moja kabla ya mchezo kumalizika.

Samuel Chukwueze aliipatia Nigeria bao la kuongoza katika dakika 45 za kwanza za pambano lililopigwa katika uwanja wa kimataifa wa michezo wa mjini Cairo.

Kocha wa Nigeria Gernot Rohr alisema baada ya mchezo kwamba ilikuwa bahati walifanikiwa kupata bao la pili lililofanikisha ushindi na akaongeza kuwa amejawa furaha kutokana na mafanikio ya timu yake kwenye mchezo wa robo fainali.

Teknolojia ya VAR yaanza kufanya kazi 

Afrika-Cup 2019 | Nigeria vs. Südafrika
Picha: Reuters/S. Hisham

Katika mchezo huo, Afrika Kusini ilisawazisha mnamo dakika ya 71 kwa goli maridhawa lililowekwa wavuni na mshambuliaji wake Bongani Zungu.

Goli hilo nusura likataliwe baada ya mshika kibendera kusema ulikuwa mpira wa kuvizia lakini hilo lilisawazishwa baadaye na teknolojia ya msaada wa vidio kwa waamuzi wa kandanda, maarufu kama VAR.

Goli la Zungu lilikuwa moja ya magoli matatu yaliyoamuliwa na teknolojia ya VAR katika siku ya kwanza ya kutumiwa teknolojia hiyo kwenye michuano ya AFCON.

Maamuzi yote matatu kuhusu magoli wakati wa mechi mbili za jana yalitoa ushindi.

Teknolojia ya msaada wa vidio kwa waamuzi wa kandanda, VAR, itaendelea kutumika katika michezo itakayopigwa leo na hadi mchezo wa mwisho wa fainali za AFCON.

Senegal yaikaba koo Benin

Africa Cup of Nations 2019 - Viertelfinale - Senegal gegen Benin | Jubel
Picha: Reuters/M. A. El Ghany

Senegal ndiyo ilikuwa timu ya kwanza kutinga hatua ya nusu fainali baada ya kuitandika Benin bao 1 kwa 0 kwenye mchezo uliopigwa katika dimba ya Juni 30 mjini Cairo.

Mabao mawili ya mshambuliaji anayechezea klabu ya Liverpool Sadio Mane yalikataliwa na teknolojia ya VAR kuwa mipira ya kuvizia.

Lakini katikati ya mbinde za kutafuta goli Idrissa Gueye aliiandikia Senegal bao la ushindi mnamo dakika ya 70 baada ya kufyetua mkwaju mkali uliompita mlinda mlango wa timu ya Benin, Owolabi Kassifa.

Vigogo wengine wa Nusu Fainali kujulikana leo 

Africa Cup 2019 Stadion in Alexandria, Ägypten
Picha: DW/A. Essam

Michezo mengine miwili ya hatua ya robo fainali itatimua vumbi baadae leo ambapo Ivory Coast atakuwa na kibarua kigumu cha kuikabili Algeria ambayo imepata sifa ya kutofungwa hata goli moja tangu kuanza kwa michuano ya AFCON.

Timu changa na iliyowashangaza wengi kwenye michuano ya mwaka huku, Madagascar, itakuwa na miadi na Tunisia katika mchezo wa kufa na kupona utakaopigwa saa nne za usiku saa za afrika mashariki.

Matokeo ya michezo hiyo ndiyo itaamua timu zitakazokutana na Senegal na Nigeria katika hatua ya nusu Fainali.

Michezo ya nusu fainali itachezwa Jumamosi ya Julai 14, na kufuatiwa na mchezo wa mshindi wa tatu utakaopigwa Jumatano ijayo ya Julai 17 na mchezo wa fainali unatarajiwa kutimua vumbi  Ijumaa ya tarehe 19 mwezi wa Julai.