Nigeria kuimarisha usalama wa safari za ndege
4 Juni 2012Rais Jonathan ameyasema hayo wakati alipolitembelea eneo la kitongoji cha mji wa Lagos, ambako ndege ya abiria ya shirika la Dana ilianguka jana na kuwaua abiria wote 153 waliokuwemo katika ndege hiyo.
"Tumekuwa tukijizatiti kuboresha sekta ya usafiri wa ndege hapa nchini. Ajali hii ni pigo kubwa kwetu na nitahakikisha ajali kama hii haitokei tena humu nchini," amesena rais Jonathan baada ya kujionea kwa macho yake uharibifu uliosababishwa na kuanguka kwa ndege hiyo.
Waziri wa usafiri wa ndege nchini Nigeria, Stella Oduah- Ogiemwonyi amesema serikali inafanyika kila linalowezekana kuepusha ajali kama hiyo katika siku zijazo. "Serikali itafanya uchunguzi wa kina kubaini kilichotokea. Hatufahamu chanzo cha ajali, lakini tunafahamu ndege ilikaribia kutua kabla marubani kuonya walikabiliwa na matatizo."
Uchunguzi watatizwa
Polisi wamefyetua gesi ya kutoa machozi kuutawanya umati wa watu waliokusanyika katika eneo la ajali. Kwa mujibu wa taarifa ya mwandishi wa habari wa shirika la AFP, polisi walilazimika kutumia vitoa machozi wakati watu takriban 2,000 walipojaribu kuingia eneo lililofungwa na polisi wakitaka kushuhudia athari za ajali hiyo na hivyo kutatiza uchunguzi.
Kufikia sasa waokoaji wamefaulu kuzitoa maiti zisizopungua 62 kutoka kwa mabaki ya ndege hiyo. Kanisa, jengo la makaazi ya watu la ghorofa mbili na duka la huduma za uchapishaji liliharibiwa vibaya katika eneo la ajali. Idadi kamili ya watu waliokufa ardhini hadi sasa haijajulikana. Moshi ungali unafuka katika eneo la ajali na malori ya zimamoto yamekuwa mbioni kuuzima moto unaoendelea kuwaka kwenye mabaki ya ndege hiyo.
Solomon Omotayo ni miongoni mwa watu walioshuhudia ndege ya shirika la Dana ikipoteza muelekeo muda mfupi kabla kuanguka katika kitongoji cha Iju jijini Lagos. "Tulipoiona, ilkuwa chini mno! Dakika kama mbili baadaye tukasikia mlio. Tuliufuata moshi hadi hapa. Maafisa waliondoa maiti lakini sijui ni ngapi. Ni hasara kubwa na maiti nyingi zingali zimefunikwa."
Shirika la safari za ndege lawamani
Mtaalamu wa safari za ndege nchini Nigeria, Rubani Mohammed Jibrin amelishutumu shirika la safari za ndege kwa rushwa usimamizi mbaya. "Ukweli ni kwamba shirika la usafiri wa anga nchini Nigeria halitimizi wajibu wake. Kuna mambo mengi yanayokwenda kombo katika shirika hilo. Kuna rushwa na ukweli unafichwa. Utoaji mafunzo na kusainiwa kwa mikataba hakufanyiki kwa njia sahihi. Ununuzi na uagizaji wa ndege kutoka nje unafanywa kiholela."
Rubani Mohammed Jibrin amemnyoshea kidole cha lawama mkurugenzi mkuu wa shirika la ndege la Nigeria Harold Demuren na kumtaka ajiuzulu mara moja ili kutoa nafasi kwa mtu mwingine aliye tayari kufanya kazi nzuri achukue nafasi yake.
Kwa upande mwingine, mkurugenzi mkuu Harold Demuren, amethibitisha kuwa rubani wa ndege hiyo alikuwa raia wa Marekani akisaidiwa na rubani mwenzake raia wa India.
Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/DPAE/APE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman