1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaNiger

Niger yapoteza wanajeshi 12 kwenye makabiliano na wanamgambo

29 Septemba 2023

Waziri wa ulinzi wa Niger Salifou Mody, amesema wanajeshi saba wameuawa siku ya Alhamisi kusini magharibi mwa nchi hiyo, katika shambulio la watu wanaoshukiwa kuwa magaidi.

https://p.dw.com/p/4Wx1K
Mwanajeshi wa Niger
Jeshi la Niger limekuwa likipambana na uasi wa itikadi kali unaoliandama eneo la kanda ya Sahel kwa miaka kadhaa sasa.Picha: ISSOUF SANOGO/AFP

Wanajeshi wengine watano wamepoteza maisha katika ajali ya barabarani walipokuwa wakijaribu kukabiliana na shambulio hilo.

Mody amesema kikosi cha jeshi kilishambuliwa vikali na magaidi wapatao 100 katika mji wa Kandadji, takriban kilomita 190 kutoka mji mkuu, Niamey karibu na mpaka wa Mali, Burkina na Niger.

Eneo la Tillaberi limekuwa kitovu cha operesheni za waasi katika ukanda wa Sahel.

Hata hivyo, Waziri Mody amesema wamefanikiwa kuwatokomeza mamia ya wanamgambo, pikipiki na zilaha zao takriban kilomita 20 kaskazini mashariki mwa Ayorou katika eneo hilo.

Hayo yanajiri wakati Ufaransa ikijiandaa kuviondoa vikosi vya kupambana na ugaidi nchini Niger, kwa ombi la utawala mpya wa kijeshi, walionyakua madaraka katika mapinduzi miezi miwili iliyopita.