Ni siku ya hukumu Marekani
6 Novemba 2012Rais Barack Obama alimalizia kampeni zake jimboni Iowa ambako ndiko alikoanzia harakati zake za kuingia ikulu ya White House miaka minne iliyopita, akiwaomba wakaazi wa jimbon hilo wamsaidie kukamilisha kile walichokianzisha miaka minne iliyopita. "Nimekuja tana Iowa kuomba ridhaa yenu kwa mara ya mwisho, nimekuja kuwaomba mnisaidie kukamilisha kile tulichokianzisha, kwa sababu hapa ndipo vuguvugu letu lilikoanzia."
Bruce Springsteen, Jay-Z wato burudani
Akisindikizwa na wanamuziki maarufu Bruce Springsteen na Jay-Z Obama alijitahidi kutetea rekodi yake katika miaka minne iliyopita. "Mnaweza kuwa hamkubaliani na kila maamuzi niliyoyafanya, mnaweza kuwa mmekatishwa tamaa na kasi ya mabadiliko niliyowaahidi huko nyuma, lakini mnajua kwamba namaanisha ninachosema na nasema ninachomaanisha," alisema Obama.
Hoja ya rais Obama katika dakika hizo za mwisho ilikuwa kwamba wapiga kura wanaweza wasimpende kwa yale yote aliyoyafanya, lakini mpinzani wake anatisha zaidi. Obama alikamilisha kampeni hiyo akiwa na matumaini ya ushindi. Kwake mkutano wa Iowa ulijaa kumbukumbu ya yaliyopita. Ushindi wake katika mkutano wa chama cha Democrats jimboni humo mwaka 2008 ndiyo iliyokuwa hatua ya kwanza katika mbio zake za urais. Na mkutano wake wa mwisho siku ya Jumatatu ulifanyika mbele ya jengo yalimokuwa makao makuu ya kampeni zake katika uchaguzi huo wa 2008.
Mitt Romney kufanya kampeni hata siku ya uchaguzi
Mitt Romney kwa upande wake aliamua kusogeza kampeni yake ya miezi 18 hadi siku ya Jumanne, ili aweze kufanya ziara tena katika majimbo muhimu ya Ohio na lile linaloegemea upande wa Democrats la Pennyslivania katika siku ya uchaguzi. Kambi yake ilisema mgombea wao ataenda katika mji wa Cleveland, jimboni Ohia na Pittsburg katika jimbo la Pennyslvania, ambalo hakulitembelea kwa zaidi ya mwezi moja hadi siku ya Jumapili.
Kampeni inasisitiza kuwa jimbo hilo sasa linaweza kuelekea kwake, hata wakati kura za maoni zinaonyesha Obama anaongoza kidogo tu katika majimbo yote yenye maamuzi. Ujumbe wa Romney kwa wapiga kura ni kwamba Obama ameshindwa na yeye ndiye atakayeweza. "Mlitarajia kuwa rais Obama atatekeleza ahadi yake kuwaleta watu pamoja na kutatua matatizo. Hajafanya hivyo, mimi nitafanya hivyo."
Kampeni siku ya uchaguzi???
Je, Kurefusha ratiba kwa Mitt Romney kutaongeza nafasi yake ya kushinda mchuano mkali na uliogharimu zaidi ya dola bilioni mbili? Jensin Johnson ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na meneja wa zamani wa kampeni za Congress: "Hakuna mtu utakayemshawishi siku ya mwisho, nadhani ni dalili kwamba Mitt Romney hajiamini vya kutosha na hajui mchuano huu utaisha vipi kwa hiyo anajaribu kila linalowezekana, sijui kama hii italeta mabadiliko yoyote lakini ndivyo nnavyoona," anasema.
Wagombea wote wanahitaji kura 270 za majimbo ili kupata ushindi. Licha ya ushindani kuwa mkali, njia ya ushindi kwa Obama ni nyepesi. Kama atashinda majimbo matatu aliyoyatembelea siku ya Jumatatu - yaani Wisconsin, Ohio na Iowa, basi atakuwa tayari amemaliza kazi.