Ni nani Muktada al-Sadr
15 Mei 2018Kutoka kupigana vita dhidi ya vikosi vya jeshi la Marekani hadi kushinda kwa kiwango kikubwa katika uchaguzi, DW inaangalia hatua za mabadiliko za Muqtada al-Sadr.
Akiunganisha Waislamu wa madhehebu ya Shia na jamii zisizo na dini chini ya kauli mbiu ya mageuzi, ushindi wa al-Sadr katika uchaguzi unaashiria kilele cha miaka ya kazi zinazolenga kupambana na rushwa pamoja na ubadhirifu katika serikali. Lakini al-Sadr alijenga jina lake katika kila kitu lakini bila ya kuingia katika siasa za nchi hiyo. Wakati vuguvugu lake la kisiasa lilivuka mipaka ya kimadhehebu kwa kubadilishana na jukwaa la uzalendo, kiongozi huyo wa kidini wa Shia ana historia ya ndani sana ya kuimarisha migawanyiko hiyo.
Hakuna mtu yeyote aliyefikia kuwa kielelezo cha mapambano dhidi ya uvamizi wa Marekani kama al-Sadr. Juni mwaka 2003, aliunda jeshi la lililovuma kwa ubaya la Mahdi kama njia ya kupambana na siku moja kuyafurusha majeshi ya uvamizi.
"Sadr aliweka wazi kwa matamshi yake na kusema kwamba alikuwa kwanza kabisa ni mzalendo wa Iraqi, ambaye hadhibitiwi na mataifa yenye nguvu ya kigeni, iwe Iran, Marekani ama nchi nyingine yoyote," alisema Thanassis Cambanis wa Wakfu wa Century wa kukusanya mawazo wiki iliyopita.
Mapambano na majeshi ya Marekani
"Matokeo yake , na hususan katika miaka ya mwanzo baada ya uvamizi, Sadr alikuwa mmoja wa makamanda wachache wa wanamgambo ambaye alipata heshima japo ya mbali kutoka makundi yote ya kimadhehebu."
Lakini wanamgambo vijana wa kiongozi huyo wa kidini walibakia kwa kiasi kikubwa chini ya uangaliazi hadi mwaka 2004, wakati walipopambana na vikosi vya majeshi ya Marekani katika mji wa kusini wa Najaf, na kusababisha kampeni kubwa iliyowalenga wanajeshi wa Marekani nchini humo.
Mwaka huo , majeshi ya Marekani yaliamuriwa kumtafuta na kumkamata akiwa hai ama amekufa baada ya jaji wa Iraq kutoa waranti wa kukamatwa kwa mauaji ya wanajeshi wa Marekani.
Kwa rais wa zamani wa Marekani George W. Bush , vitendo vya al-Sadr na wafuasi wake vilifikia katika kile alichosema kuwa ni kupinga demokrasia.
Jeshi la Mahdi halikuwalenga tu wanajeshi wa Marekani. Katika kipindi chake cha mapambano , wanamgambo hao pia waliwalenga Wairaqi wa madhehebu ya Sunni na makundi mengine ya Washia. Jeshi hilo lilishutumiwa kwa kufanya mauaji kwa kuunda vikosi vya mauaji , na kwa kufanya hivyo wakachochea mivutano ya kimadhehebu.
Iliofika mwaka 2006 , jarida la habari la Marekani Newsweek lilimuweka al-Sadr katika ukurasa wa mbele na kumpa jina la "mtu hatari zaidi nchini Iraq."
Kundi hatari zaidi
"Kundi hilo lilikuja kuangaliwa katika maeneo mengi ya Iraq kuwa hatari zaidi kuliko kundi la al-Qaeda nchini Iraq na la pili kwa vikosi vya Marekani kwa uwezo na nguvu za kijeshi," kwa mujibu wa mradi wa kuangalia maeneo ya wanamgambo katika chuo kikuu cha Stanford.
Hata hivyo , jeshi la Mahdi lilianza kupoteza uungwaji mkono mwaka 2007 , baada ya mahujaji wa Kishia 50 kuuwawa katika mapambano na kundi jingine la wanamgambo wa Kishia katika eneo la Karbala. Mwaka uliofuatia , al-Sadr aliamuru wanamgambo wake kuweka silaha zao chini. Wakati baadhi ya wapiganaji walichukuliwa kuingia katika jeshi la serikali, wengine walipewa jina la Mumahidoon na kuelekeza nguvu zao katika huduma za jamii kama masomo ya Qurabi, ujenzi katika halmashauri na kukusanya taka katika maeneo ya Washia.
Mwaka 2008 , al-Sadr alikwenda Iran, ambako alibaki huko akiishi uhamishoni. Hata hivyo , aliendelea kuongoza vuguvugu la Sadr na kutumia mamlaka yake kushawishi hali ya kisiasa nchini Iraq.
Mwaka 2011, al-Sadr alirejea nchini Iraq ili kuwa na usemi mkubwa katika siasa za nchi hiyo. Mwishoni mwa mwaka huo , majeshi ya Marekani yalikamilisha kujitoa nchini Iraq, na kukamilisha dai kuu la al-Sadr.
Mwandishi: Kersten Knipp / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman