1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

Ngungunyane: mfalme dhidi ya utawala wa Kireno

25 Julai 2018

Ulishawahi kumsiki Mfalme Ngungunyane aliyeongoza ufalme wa Gaza ambao hata baada ya wakoloni kuligawa bara la Afrika, ufalme huo haukuguswa? Basi sikia historia yake hapa, ambayo inamtaja kuwa mwanadiplomasia makini aliyekuwa na uwezo wa kuwagonganisha hata hao wakoloni wenyewe kwa wenyewe.

https://p.dw.com/p/2woua

Ni wapi na wakati gani Ngungunyane aliishi? Ngungunyane, alipewa jina Mudungazi, alipozaliwa takriban mwaka 1850 katika himaya ya kusini mashariki ya ufalme wa Gaza. Babu yake Manukuse alikuwa na himaya kubwa kuanzia mto Incomati iliyoko kusini na Bahari Hindi mashariki hadi mto Zambezi na mto Save iliyoko kaskazini, eneo ambalo leo hii ni taifa la Msumbiji na baadhi ya sehemu ya mataifa jirani. Baadaye Ngungunyane alikuja kuwa mfalme wa mwisho wa Gaza kabla ya ufalme wake kushindwa na Wareno. Aliaga dunia Desemba, 23 mwaka 1906, katika kisiwa cha Terceira alikohamishwa.

Je, Ngungunyane alipata vipi madaraka? Baada ya kifo cha babu yake Ngungunyane,  Manukuse, mwaka 1858, Muzila alishinda vita vya urithi kati ya warithi wawili huku akisaidiwa na mamlaka ya Ureno. Urithi wake ulikuwa na matatizo. Mwana wa Muzila na mke aliyempenda Yosio, Mudungazi aliamuru kuuawa kwa mmoja wa ndugu zake na kuingia usukani mwaka 1884. Alibadilisha jina lake na kuwa Ngungunyane, "yule mbaya" ama "asiyeoonekana". Kwa miaka 11, alitawala kiimla akitumia ghasia kuwakabili watu waliokuwa wakisimamia vipande vya ardhi. 

Ngungunyane alihusiana vipi na Wazungu? Ngungunyane alichukua mamlaka miezi michache baada ya kufanyika kwa kongamano la Berlin (1884-85), wakati mataifa ya Ulaya yalipoligawanya bara la Afrika miongoni mwao. Huku Uingereza na Ujerumani yakikabiliwa na tamaa, kwa himaya za Msumbiji, Ureno ilishinikizwa kutwaa ufalme wa Gaza. 
Alipotambua ushindani kati ya mataifa ya Ulaya, Ngungunyane alijaribu kuchukua fursa hiyo na kufanya urafiki na mataifa tofauti yakiwemo Uingereya na Ureno. 

Ngungunyane alishindwa vipi? Mapema mwaka 1895, Balozi António Eanes, nchini Msumbiji aliamuru wanajeshi kumkabili Ngungunyane. Wakati huo, Ngungunyane alikuwa amepoteza Imani kwa wafusia wake watiifu. Ufalme wake ulishindwa vibaya na umwagikaji mkubwa wa damu kushuhudiwa kwenye majkabiliano hayo. Baada ya vita katika maeneo ya Coolela na Mandlakasi, Ngungunyane alitorokea Chaimite, eneo takatifu ambalo babu yake alizikwa. Tarehe 28 mwezi Desemba mwaka 1895, alitiwa nguvuni na gavana Mouzinho de Albuquerque wa wilaya ya kijeshi ya Gaza. Alipewa uhamisho katika mji mkuu wa Uren, Lisbon. Ngungunyane na msafara wake ulidhihakiwa kabla ya kufanyiwa maonyesho katika bustani ya Belem Botanic.

Ngungunyane aliishi Ureno maisha yake yote baada ya kuhamishwa. Alilazimishwa kusoma na kuandika na kisha kulazimishwa kuwa Mkristo, akabatizwa akapewa jina, Reinaldo Frederico Gungunhana.  “Simba wa Gaza” alikufa Desemba 23 mwaka 1906 kutokana na kufuja damu ubongoni.

Asili ya Afrika: Ngungunyane

Ni, vipi Ngungunyane alikuwa shujaa kwenye mapambano dhidi ya mkoloni? Kufuatia ombi la rais wa kwanza wa Msumbuji Samora Machel, kipande cha ardhi kilinunuliwa katika eneo la Azores, kama ishara ya kumuenzi na kumzika Ngungunyane. Marehemu aliletwa Maputo mwaka 1985, kwa muongo wa 10 wa kuadhimisha uhuru Msumbiji. 

Kwa FRELIMO (Mozambique Liberation Front vugu vugu ambalo lilipigania uhuru wa Msumbiji na chama tawala tangu uhuru mwaka 1975), Ngungunyane mara nyingi alionekana kuwa shujaa na chanzo cha kutia moyo wakati wa vita vya ukombozi na pia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Watu mashuhuri katika siasa za Msumbiji walitokea katika mkoa wa Gaza alikotokea Ngungunyane: Eduardo Mondlane, mwasisi wa chama cha FRELIMO na rais wa kwanza  Samora Machel na Joaquim Chissano, rais wa pili wa Msumbiji.

Je, Ngungunyane alikuwa mtu mwenye utata? Kumbukumbu ya Ngungunyane ililenga kuelimisha vizazi vipya kuwa wazalendo nchini Msumbiji na kunadi umoja wa taifa. Lakini mpango huo hukufaulu: Karne moja baada ya kushindwa, vita vya ukombozi vya Ngungunyane dhidi ya mkoloni viligubikwa na dhulma kwa waliotawaliwa naye. Mwaka 1995, wakiadhimisha miaka 100 ya vita vya ukombozi vya Gaza, rais wa zamani wa Msumbiji Joaquim Chissano, alizindua sanamu ya Ngungunyane katika eneo la Mandlakazi, mkoani Gaza. Hata hivyo siku chache baadaye wakaazi waliivunja. Taswira hiyo inaonyesha utata wa urithi wa Ngungunyane: Anasalia kuwa mtu ambaye alipendwa na baadhi ya watu na wengine kumchukia.

Gloria Sousa, Romeu da Silva na Gwendolin Hilse  wamechangia katika makala hii. Ni sehemu ya makala maalum za  mfululizo wa "Asili ya Afrika", ushirikiano kati ya shirika la DW na taasisi ya Gerda Henkel.

Mwandishi: Glória Sousa, Romeu da Silva na Gwendolin Hilse
Imetafsiriwa na: Shisia Wasilwa
Mhariri: Iddi Ssessanga