1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiAfrika

Ngozi Okonjo-Iweala mwanamke aliyeleta fahari Afrika

Josephat Charo
16 Februari 2021

Ngozi Okonjo-Iweala ameteuliwa kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya mkuu wa shirika la biashara la kimataifa WTO. Raia huyo wa Marekani mwenye asili ya Nigeria amekuwa akitetea na kuendeleza biashara na maendeleo.

https://p.dw.com/p/3pRBq
Ehemalige Außen- und Finanzminister Ngozi Okonjo-Iweala
Picha: Fabrice Coffrini/AFP

Ngozi Okonjo-Iweala ni msomi, mchumi na mtaalamu wa masuala ya fedha ya kimataifa na maendeleo. Anachukuliwa kuwa mzungumzaji mwenye ujuzi wa kushawishi na kupatanisha, na mbinu za kupata makubaliano au muafaka baina ya pande mbalimbali, baada ya kujikusanyia ujuzi mkubwa barani Afrika, Asia, Ulaya, Amerika Kusini na Amerika Kaskazini.WTO kuongozwa na mchumi kutoka Afrika

Ngozi, mwenye umri wa miaka 66 ni mwenyekiti wa muungano wa chanjo wa GAVI na ni mwanachama wa bodi ya mtandao wa kijamii wa twitter. Hivi karibuni aliteuliwa kuwa mjumbe maalumu wa Umoja wa Afrika kusimamia mipango na mikakati ya bara hilo kufikia misaada kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.

Bundesliga I FC Bayern Muenchen v DSC Arminia Bielefeld
Ngozi Okonjo-Iweala mkuu mpya wa WTOPicha: Gian Ehrenzeller/KEYSTONE/dpa/picture alliance

Ngozi Okonjo Iweala alitumia miaka 25 kama mchumi katika masuala ya maendeleo kwenye benki ya dunia, ambapo alipanda ngazi kwa kasi hadi kuwa mkurugenzi mtendaji aliyehusika na shughuli za benki hiyo. Alianzisha miradi kadhaa ya benki ya dunia kuzisaidia nchi zenye kipato cha chini wakati wa mizozo ya uhaba wa chakula na uchumi iliyoikabili dunia, akisaidia kuleta faida ya zaidi ya dola bilioni 40 kwa shirika la maendeleo la kimataifa, IDA, ambalo ni kitengo cha benki ya dunia kinachoshughulikia utoaji wa misaada ya fedha na mikopo.

Okonjo-Iweala alihudumu mara mbili kama waziri wa fedha wa Nigeria kati ya 2003-2006 na 2011-2015 na kwa muda mfupi akawa kaimu waziri wa mambo ya nchi za nje mnamo mwaka 2006. Alikuwa mwanamke wa kwanza wa Nigeria kushika nyadhifa zote mbili.

Kama waziri wa fedha, Okonjo-Iwela alitekeleza mpango wa mageuzi mapana ya kiuchumi yaliyochangia pakubwa kuleta uthabiti kwa uchumi wa Nigeria, kuongeza mara tatu kasi ya ukuaji na kuimarisha uwazi katika kufanya miamala ya fedha kwa lengo la kupambana na ufisadi. Wanigeria wanamuona Okonjo-Iweala kama mwanamke aliyeikomboa nchi yao na kuukwamua uchumi uliokuwa umelemaa.

Alipokuwa waziri wa fedha wa Nigeria, Okonjo-Iweala aliongoza mazungumzo ya Nigeria na wakopeshaji wa kimataifa, ambayo mnamo mwaka 2015 yalizaa matunda wakati deni la Nigeria la dola bilioni 30 liliposamehewa, ikiwa ni pamoja na kufutwa kabisa moja kwa moja kwa dola bilioni 19.

Okonjo-Iweala anajieleza mwenyewe kama muamini thabiti katika nguvu za biashara kuzinyanyua nchi zinazoendelea kuondokana na jinamizi la umasikini.

Kombobild | Ngozi Okonjo-Iweala und Yoo Myung-hee
Alikuwa akichuana kwa karibu na Yoo Myung-hee wa Korea Kusini

Alipata shahada ya uchumi katika chuo kikuu cha Havard nchini Marekani mwaka 1976, shahada ya uzamili kutoka chuo cha teknolojia cha Massachusetts na akatunukiwa shahada 15 za heshima kutoka vyuo mbalimbali kote ulimwenguni.

Okonjo-Iweala ni mwandishi wa vitabu kadhaa na makala kuhusu fedha na uchumi.

Mnamo mwaka 2019, shirika la kimataifa la kupambana na rushwa, Transparency International lilimtaja kuwa miongoni mwa wanaharakati wanane wanawake wanaopambana dhidi ya rushwa.

Mwaka 2015 jarida la Fortune lilimtaja kuwa miongoni mwa viongozi 50 wenye haiba kubwa duniani. Mwaka 2014 jarida la Time lilimuorodhesha kuwa miongoni mwa watu 100 wenye ushawishi mkubwa kabisa ulimwenguni.

Okonjo-Iweala ameolewa na ana watoto wanne na wajukuu watatu.