NEW YORK.Uvamizi wa Israel katika ukanda wa Gaza walaaniwa na baraza la haki za binadamu la umoja wa mataifa
6 Julai 2006Baraza la haki za binadamu la umoja wa mataifa limeilaani hatua ya Israel ya kuushambulia kijeshi ukanda wa Gaza.
Uamuzi huo umefuatia mashambulio ya helikoipta za jeshi za Israel katika eneo la Palestina kwa siku tisa mfululizo.
Katika eneo la Beit Lahiya kaskazini mwa Ukanda wa Gaza majeshi ya Israel yamewauwa wapalestina wanne kwa kuwapiga risasi katika katika mapambano baina ya wanajeshi wa Israel na raia wa Palestina kwa mara ya kwanza tangu wanajeshi wa Israel walipoingia katika ukanda wa Gaza.
Baraza la haki za binadamu la umoja wa mataifa limesema kwamba litawapeleka wachunguzi wake katika eneo la mashariki ya kati..
Mapema leo majeshi ya Israel yaliingia ndani zaidi ya kaskazini mwa Gaza na kuichukua sehemu yenye makaazi matatu iliyokuwa zamani inakaliwa na walowezi wa kiyahudi.
Jeshi la Israel limearifu kuwa limeweka vifaru katika sehemu hiyo kufuatia mashambulio ya makombora yaliyofanywa na wapiganaji wa kipalestina kuelekezwa katika mji wa israel wa Ashkelon.
Israel inatumia hatua za kijeshi kushinikiza kuachiliwa kwa mwanajeshi wake aliye tekwa nyara mwezi uliopita.