1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK.Shirika la kudhibiti nishati lasema kuna dalili za madini ya Uranium yaliyorutubishwa nchini Iran

15 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCsU

Shirika la kimataifa la kudhibiti nishati ya nyuklia limesema kuwa dalili za madini ya Uranium yaliyorutubishwa zimegunduliwa nchini Iran lakini shirika hilo limeshindwa kueleza kwa kina juu ya dalili hizo mpya.

Katika ripoti yake shirika hilo la kimataifa la kudhibiti nishati ya nyuklia limeeleza kuhusu Iran na inavyo endeleza shughuli zake za utafiti wa kurutubisha madini ya Uranium.

Nchi za magharibi zinahofia kuwa nchi hiyo huenda ikatengeneza silaha za nyuklia.

Licha ya tishio la kuiwekea vikwazo Iran rais wa nchi hiyo Mahmoud Ahmednejad ametangaza kuwa nchi yake imeazimia kukamilisha mpango wake wa nishati ya nyuklia kufikia mwisho wa mwezi machi mwakani, ambao ndio mwisho wa mwaka kwa mujibu wa kalenda ya Iran.

Wakati huo huo waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert ametowa mwito kwa jamii ya kimataifa ichukuwe hatua dhidi ya tamaa ya nyuklia kwa Iran.

Bwana Olmert ambae anakamilisha ziara yake nchini Marekani pia amezitaka nchi za kiarabu zenye msimamo wa kadiri kuungana dhidi ya Iran ili kuzuia machafuko katika mashariki ya kati.