NEW YORK:Marekani na Uingereza kukutana na Annan
9 Januari 2004Matangazo
Mabalozi wa Marekani na Uingereza leo hii watakuwa na mashauriano na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan kabla ya kufanyika kwa mkutano muhimu juu ya dhima ya Umoja wa Mataifa nchini Iraq katika kipindi cha usoni. Nchi hizo zote mbili zinataka Umoja wa Mataifa kumrudisha nchini Iraq mfanyakazi mwandamizi wa kisiasa.Uingereza imekuwa ikiutaka Umoja wa Mataifa isaidie uteuzi wa bunge la mpito kabla ya kukabidhiwa madaraka kwa Wairaq mwishoni mwa mwezi wa Juni. Lakini maafisa wa Umoja wa Mataifa wanataka wapatiwe dhima ilio wazi ya kujitegemea kwa chombo hicho nchini Iraq wakati huo huo ikiwa na wasi wasi wa kutuma wafanyakazi wake nchini kote Iraq na hadi sasa maafisa wake wamekuwa wakiendesha shughuli zao kwa kwenda na kurudi nchini humo wakitokea Jordan na Cyprus. Umoja wa Mataifa uliwaondosha wafanyakazi wake wa kimataifa hapo mwezi wa Oktoba baada ya mashambulizi ya mawili ya mabomu katika makao makuu yake nchini Iraq kupelekea vifo vya wafanyakazi 22 pamoja na watu waliokuwa wametembelea makao makuu hayo. Tokea wakati huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan amekuwa akisisitiza kwamba hatowarudisha nchini humo wafanyakazi wake hadi hapo hali ya usalama itakapoimarishwa na dhima ya Umoja wa Mataifa nchini humo itakapofafanuliwa vyema katika kuchangia mustakabli wa nchi hiyo.
Matangazo