NEW YORK:Kofi Annan aitaka jumuiya ya kimataifa kulishughulikia suala la Darfur
20 Desemba 2006Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeondoka Kofi Annan ametoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa kulishughulikia haraka suala la mzozo wa Darfur magharibi mwa Sudan.
Bwana Annan ameyasema hayo alipofanya mkutano wake wa mwisho na waandishi wa habari kama katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Akizungumzia mambo ambayo hatoyasahau katika kipindi chake kama katibu mkuu alisema ni wakati Marekani ilipoanzisha vita dhidi ya Iraq pamoja na ile kashfa ya mpango wa umoja wa mataifa wa chakula kwa mafuta nchini Iraq kashfa ambayo ilimhusisha mwanawe.
Bwana Annan pia ametoa mwito kwa baraza la usalama la Umoja huo kutafuta njia mwafaka ya kusuluhisha mvutano juu ya Iran akionya kwamba hatua yoyote ya Kijeshi dhidi ya Iran itasababisha janga kubwa.
Matamshi hayo ya Annan yamekuja wakati ambapo kuna taarifa kwamba Marekani inataka Umoja wa mataifa kupiga kura haraka juu ya kuiwekea vikwazo Iran.