1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

New York.Baraza la Usalama kutuma wanadiplomasia huko Ethiopia.

10 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCuH

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kutuma wanadiplomasia wawili mjini Addis Ababa siku ya Jumatatu, ili kufanya mazungumzo na serikali ya Sudan na Umoja wa nchi za Kiafrika (AU) kuhusiana na mgogoro wa jimbo la Darfur.

Akizungumza na muandishi wa habari kwa sharti la kutotajwa jina, mwanadiplomasia mmoja amesema, wanadiplomasia wawili kutoka nchi 15 wanachama wa baraza hilo, watasafiri kuelekea mji mkuu wa Ethiopia kunako makao makuu ya Umoja wa Afrika.

Baraza la Usalama liliamua tarehe 31 mwezi August, kupeleka kikosi imara cha jeshi la Umoja wa Mataifa kitakachokuwa na wanajeshi 20,000 nchini Sudan katika jimbo lililoharibika kwa vita la Darfur, ili kuchukua nafasi ya vikosi vya Umoja wa Afrika vilivyoishiwa fedha na vyenye vifaa duni vya kufanyia kazi, na ambavyo vimevyoshindwa kusimamisha umwagaji wa damu katika jimbo hilo.

Hata hivyo Rais wa Sudan Omar al-Bashir ameupinga mpango huo wa kupelekwa jeshi kama hilo, ambao mwenyewe anauona kama ni sehemu ya nchi za Magharibi kutaka kuitawala nchi yake na kutaka kujichukulia mafuta na mali ghafi nyengine zilizomo nchini humo.

Inakisiwa kuwa watu kiasi cha 200,000 wameuwawa na wengine milioni 2.5 hawajulikani walipo, tangu kuanza mzozo wa jimbo hilo.