NEW YORK Umoja wa mataifa walaani ubakaji barani Afrika
22 Juni 2005Umoja wa mataifa umelaani vitendo vya ubakaji vinavyofanywa katika maeneo yaliyokumbwa na mizozo barani Afrika. Afisa mkuu wa misaada wa umoja huo, Jan Egeland, amesema ubakaji unatumiwa kama silaha inayopendwa katika maeneo hayo. Aliyasema hayo wakati alipokuwa akilihutubia baraza la usalama la umoja wa mataifa, juu ya kushidhwa kwa juhudi za kuwalinda raia wanaokumbwa na mizozo ya vita.
Ameongeza kusema kwamba wanawake na watoto ndio wanaoathiriwa na vitendo hivyo na kuchukiwa na jamii zao, huku wabakaji wakiachwa huru pasipo kuchukuliwa hatua yoyote.
Egeland amezitaja Sudan na jamhuri ya kidemokrasi ya Congo kama mataifa mawili ambamo ubakaji umekithiri. Shirika moja la kutoa huduma za matibabu limewatibu wanawake na wasichana 500 waliohujumiwa katika eneo la Darfur, katika kipindi cha miezi minne, ikiwa ni sehemu tu ya idadi halisi.