1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

New York. Mkutano wa kuunda jeshi la kulinda amani Lebanon kesho.

2 Agosti 2006
https://p.dw.com/p/CDPd

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Kofi Annan amesema jana kuwa mataifa ambayo yako tayari kuchangia wanajeshi katika jeshi la kulinda amani kusini mwa Lebanon yatakutana kesho Alhamis.

Annan ametoa tamko hilo kufuatia mkutano wake na mabalozi kutoka katika nchi tano wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la umoja wa mataifa, ambayo ni Uingereza, China, Ufaransa, Urusi na Marekani.

Mkutano huo wa kesho utakuwa chini ya uenyekiti wa katibu mkuu msaidizi wa umoja wa mataifa kwa ajili ya masuala ya kulinda amani, Jean-Marie Guehenno.

Wakati huo huo viongozi wa kidini wa Kikristo, madhehebu ya Kiislamu ya Sunni na Shia nchini Lebanon wametoa taarifa ya pamoja juu ya hali ya mambo katika mashariki ya kati.

Wameishutumu Israel kwa uhalifu wa kivita na kwa upande mwingine wameishutumu Hizbollah kwa kujifanya kuwa taifa ndani ya taifa kusini mwa Lebanon.

Hiyo ni taarifa ya kwanza ya pamoja ya viongozi hao wa kidini katika muda wa miaka 10.