NEW YORK-Mataifa ya Magharibi yapokea kwa hadhari tangazo la Syria kumaliza kuwaondoa wanajeshi wake wote kutoka Lebanon.
27 Aprili 2005Viongozi wengi wa nchi za Magharibi wamelipokea kwa hadhari,tangazo la Syria la kumaliza kazi ya kuwaondoa wanajeshi wake wote kutoka Lebanon.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Kofi Annan,amesema bado hawezi kuthibitisha kauli ya Syria ya kuondoka Lebanon,hadi timu yake ya kiufundi itakapomthibitishia.
Serikali mjini Damascus iliuarifu Umoja wa Mataifa kuwa imemaliza kazi ya kuwandoa wanajeshi wake wote waliokuwa katika nchi jirani ya Lebanon jana siku ya Jumanne.Hatua hiyo imemaliza kipindi cha miaka 30 cha majeshi ya Syria kuwepo Lebanon.Pia uamuzi huo unaonekana kuiweka karibu Syria na Umoja wa Mtaifa kuelekea kusimamishwa kwa azimio la Umoja huo linalotaka kuondolewa kwa majeshi yote ya kigeni kutoka Lebanon.
Shinikizo la kimataifa kwa Syria kuondosha majeshi yake lilianza mara baada ya kutokea mauaji ya Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon,Rafik Hariri miezi miwili iliyopita.
Walebanon wengi wanaamini kuwa mauaji ya Bwana Hariri yalikuwa na mkono wa Syria.