1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK. Lebanon yashinikizwa kufanya uchaguzi mkuu.

5 Mei 2005
https://p.dw.com/p/CFGS

Baraza la usalama la umoja wa mataifa linaendelea kuishinikiza Lebanon kufanya uchaguzi mkuu, likisema ni muhimu uchaguzi huo kufanyika mwezi huu kama ilivyopangwa. Baraza hilo limeitaka serikali ya Beirut kuomba msaada kutoka kwa jamii ya kimataifa kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa njia huru na ya haki, ili matokeo yake yaweze kukubalika na kuidhinishwa.

Katika taarifa iliyotolewa, mataifa yote 15 wanachama wa baraza la usalama yalimuunga mkono katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Kofi Annan, kwa kusisitiza uchaguzi wa Lebanon ufanyike tarehe 29 mwezi huu wa Mei. Uchaguzi huo utakuwa wa kwanza kufanyika tangu wanajeshi wa Syria kuondoka kutoka Lebanon.

Annan amewatuma wajumbe wake kuthibitisha kuondoka kwa wanajeshi hao wa Syria na maofisa wawili wa uchaguzi wa umoja wa mataifa wanatarajiwa kuwasili nchini humo kabla juma hili kumalizika.