NEW YORK: Azimio juu ya Lebanon kupigiwa kura kesho
8 Agosti 2006Ufaransa na Marekani zinajaribu kulifanyia marekebisho azimio la Umoja wa Mataifa linalonuia kumaliza vita kati ya Israel na kundi la Hezbollah, kufuatia hatua ya jumuiya ya nchi za kiarabu kulikosoa vikali azimio hilo.
Huku mapigano yakiendelea kuchacha, Marekani inaonekana haina nia ya kulibadili azimio hilo, lakini imekubali mawaziri wa mambo ya kigeni wa jumuiya ya nchi za kiarabu wawasilishe mapendekezo yao katika kikao maalumu cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa hii leo mjini New York.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, John Bolton, amesema bado wanajadili juu ya vipengele vinavyoweza kuongezwa katika azimio hilo kulingana na yanayoendelea nchini Lebanon.
Lebanon ililikataa azimio lililopendekezwa kwa sababu haliitishi kuondoka kwa wanajeshi wa Israel kutoka eneo la kusini. Azimio hilo linatarajiwa kupigiwa kura hapo kesho.