New York. Annan aionya Sudan kwamba itawajibika kutokana na mauaji ya Darfur.
8 Desemba 2006Katibu mkuu wa umoja wa mataifa anayeondoka madarakani Kofi Annan ameionya serikali ya Sudan kuwa itawajibika kuchukua dhamana kwa jumla kuhusiana na uhalifu uliofanywa katika jimbo la Darfur. Annan amesema kuwa serikali ya Khartoum imekataa kukubali msaada kutoka katika jumuiya ya kimataifa ili kuzuwia mauaji, ubakaji na uharibifu wa vijiji katika jimbo hilo la magharibi ya nchi hiyo.
Katibu mkuu amemkumbusha rais Omar al-Bashir kuwa katika mkutano mwezi Novemba mjini Abuja , viongozi wa Afrika ikiwa ni pamoja na Bashir , walikubaliana kuhusu ujumbe wa nyongeza wa umoja wa mataifa , ili kuimarisha kikosi cha sasa cha mataifa ya Afrika cha kulinda amani ambacho kina wanajeshi 7,000 katika jimbo la Darfur. Tangu wakati huo , Bashir amesema kuwa umoja wa mataifa unaweza kutoa msaada tu kwa jeshi la sasa la umoja wa Afrika. Tangu mapema 2003, wanamgambo wanaoungwa mkono na serikali na waasi wamekuwa wakipigana vita ambavyo vimesababisha watu 200,000 kupoteza maisha.