NEW YORK: Angola yashutumiwa kwa kuficha fedha
13 Januari 2004Matangazo
Shirika la Kutetea Haki za Binaadamu lenye makao yake mjini New York Marekani la Human Right Watch limeishutumu serikali ya Angola kwa kuficha dola bilioni nne za mapato ya mafuta ambazo zingeliweza kutumiwa kupunguza umaskini na magonjwa. Shirika hilo linadai kwamba fedha hizo zilitoweka kutoka hazina za serikali kuanzia mwaka 1997 hadi mwaka 2002 na kutaka misaada zaidi kwa nchi hiyo iwekewe masharti makali ya kuwepo kwa uwazi katika nchi hiyo.Mwezi uliopita balozi wa Angola mjini Washington amesema matumizi ya kijamii yataongezeka nchini humo hadi kufikia asilimia 33 ya bajeti ya Angola. Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Angola vilimalizika hapo mwaka 2002 na kuwaacha Waangola 900,000 bila ya makaazi.Mamilioni ya wananchi wake wana uwezo mdogo wa kuzifikia huduma za matibabu na kuweza kwenda shule. Wiki iliopita Umoja wa Ulaya uliidhinisha euro 900,000 kwa ajili ya kuwapatia wananchi wa nchi hiyo makaazi mapya.