1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu kuunda serikali ya siasa za mrengo wa kulia

11 Aprili 2019

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anaanza leo mchakato wa kuunda serikali ya muungano ya siasa za mrengo wa kulia baada ya kupata ushindi katika uchaguzi

https://p.dw.com/p/3GbQ6
Israel Wahlen Wahlparty Netanjahu
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Schalit

Matokeo ya uchaguzi wa Jumanne yamekuja licha ya tuhuma za ufisadi dhidi ya Netanyahu mwenye umri wa miaka 69 na kumuweka kwenye mkondo baadaye mwaka huu wa kuwa waziri Mkuu wa muda mrefu zaidi katika historia ya Israel.

Mshirika wake wa karibu Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye ameigeuza sera ya nchi yake kwa kumuunga mkono waziwazi Netanyahu, amesema ushindi wa waziri mkuu huyo wa kuongoza kwa muhula wa tano unaupa mpango wa Amani wa Ikulu ya Marekani nafasi nzuri ya kutekelezwa.

Chama cha Netanyahu cha siasa za mrengo wa kulia cha Likud kinaonekana kupata idadi sawa ya viti bungeni na muungano wa siasa za wastani wa Bluu na Nyeupe unaoognozwa na mpinzani wake, mkuu wa zamani wa jeshi Benny Gantz.

Lakini matokeo yalionyesha kuwa Likud pamoja na vyama vingine vya siasa za mrengo wa kulia vinavyomuunga mkono waziri mkuu vitakuwa na karibu viti 65 kwenye bunge la Israel lenye viti 120.

Israel Wahlen Kahol Lavan Jubel Gantz
Benny Gantz amekiri kushindwaPicha: Reuters/A. Cohen

Akizungumza na waandishi wa habari jana usiku, Gantz alikiri kushindwa akisema kuwa wanaheshimu uamuzi wa umma. Matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa ifikapo kesho Ijumaa.

Waziri wa zamani wa fedha Yair Lapid, ambaye ni mwenyekiti mwenza wa muungano wa Bluu na Nyeupe, aliapa kuikabili vilivyo serikali ya Netanyahu- "Nnakifahamisha mapema chama cha Likud, Netanyahu na serikali ya muungano. Tutayafanya maisha yenu kuwa magumu. siku ambazo upinzani ulinyamazishwa na serikali zimeisha. Tutadai uchunguzi wa serikali kuhusu suala la nyambizi, hatutaacha kuendelea na mashitaka dhidi ya Netanyahu. Tutaligeuza bunge kuwa uwanja wa mapambano". Alisema Yair

Matokeo hayo yanamlazimu Rais Reuven Rivlin, ambaye lazima amuombe mmoja wa wagombea hao kuunda serikali, kumteua Netanyahu.

Mazungumzo makali ya kuunda serikali ya muungano huenda yakachukua siku kadhaa au hata wiki kadhaa. Rivlin amesema ataanzisha mazungumzo na viongozi wa vyama wiki ijayo kabla ya kufanya uamuzi. Ofisi yake imesema mashauriano hayo yatatangazwa moja kwa moja kwa mara ya kwanza nchini humo.

Washirika wengine wa Netanyahu wakiwemo Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, Naibu Waziri Mkuu wa Italia Matteo Salvini na Kansela wa Austria Sebastian Kurz pia walituma salamu zao za  pongezi.