1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu asema Israel itapigana kufa kupona hadi ishinde

10 Mei 2024

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kitisho cha Marekani cha kutoipatia silaha, hakitoizuia nchi yake kuendeleza mashambulizi katika Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4fhHm
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Netanyahu amesema kitisho cha Marekani cha kutoipatia silaha, hakitoizuia Israel kuendeleza mashambulizi GazaPicha: Menahem Kahana/AFP

Matamshi hayo yanaashiria kwamba Israel ina uwezekano wa kusonga mbele na uvamizi wake katika mji wa Rafah, tofauti na matakwa ya mshirika wake mkuu Marekani.

Rais Joe Biden ameitaka Israel kutoendelea namipango yake ya kuishambulia Rafah, kwa hofu ya kuzidisha janga la kibinadamu. Biden alisema kwamba Marekani haiwezi kutoa silaha kwa ajili ya operesheni ya Rafah. Lakini katika taarifa aliyoitoa jana, Netanyahu alisema kuwa wako tayari kupigana kufa na kupona hata kama hawatoungwa mkono. "Ikiwa Israel italazimika kusimama yenyewe, tutafanya hivyo. Lakini pia tunajua kwamba hatuko peke yetu, tunao watu wengi wazuri kila mahali wanaotuunga mkono, ambao wanaelewa ukweli na tutawashinda maadui zetu na kulinda mustakabali wetu wa baadae".

Wakati huo huo Israel imefanya mashambulizi mapya yaliyoulenga mji wa Rafah mapema Ijumaa. Hayo yanajiri wakati wasuluhishi wanaofanya mazungumzo kuhusu masharti ya usitishaji vita Gaza wakiondoka Cairo katika kile Misri ilichokitaja kuwa ni mazungumzo ya siku mbili yasiyo ya moja kwa moja.