Netanyahu adai kupata ushindi katika uchaguzi wa Israel
3 Machi 2020Hii ina maana kuwa Netanyahu anaelekea kushinda muhula wa tano madarakani licha ya kesi ya ufisadi inayomkabil, inayotarajiwa kuanza Machi 17
Tume ya Uchaguzi ya Israel imetangaza sehemu ya matokeo ya mwanzo yakionyesha chama tawala cha kihafidhina cha Netanyahu, Likud kimeshinda asilimia 28.72 ya karibu thuluthi moja ya kura zilizohesabiwa, dhidi ya asilimia 23.26 ya muungano wa siasa za wastani wa Blue and White wa mpinzani wake mkuu Benny Gantz. Tume hiyo ya uchaguzi imesema kucheleweshwa kwa shughuli ya kuhesabu kura kumetokana na idadi kubwa ya wapiga kura waliojitokeza ya asilimia 71. Netanyahu ameyaita matokeo ya uchaguzi huo kuwa "ushindi mkubwa” wakati akiwahutubia wafuasi wake mjini Tel Aviv mapema leo.
Matokeo ya uchunguzi wa maoni ya waliopiga kura yaliyochapishwa baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa saa nne usiku yalionyesha chama cha Likud kikikadiriwa kuwa na uongozi wa pengo la viti vine hadi vitano dhidi ya Blue and White – ikiwa ni pengo kubwa Zaidi kuliko utabiri wowote mwingine uliochapishwa kabla ya uchaguzi huo wa jana.
Kundi la Netanyahu la vyama vya siasa za mrengo wa kulia na kidini, hata hivyo kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi wa maoni ya waliopiga kura, kinashinda jumla ya viti 59 katika bunge la Knesset, ikiwa ni pungufu ya viti viwili ili kupata wingi wa viti unaohotajika kuunda serikali. "Nilizungumza awali na viongozi wote wa vyama vya kundi la siasa za mrengo wa kulia, washirika wetu wa asili. Baada ya kupata usingizi kidogo, tutakutana tena ili kuanza kuunda haraka iwezekanavyo serikali yenye nguvu na thabiti, serikali nzuri ya kitaifa kwa ajili ya taifa la Israel.
Gantz alielezea kusikitishwa kwake na matokeo hayo na kuwatuhumu wapinzani wa kisiasa kwa kusambaza uwongo dhidi yake. Amesema uchaguzi huo ndio uliokuwa na kampeni chafu Zaidi katika historia ya Israel. "Ninatambua na kuwa na hisia za maumivu na kukatishwa tamaa kwa sababu haya sio matokeo ambayo labda tulitaka kuyaona na kama haya ndio matokeo yenyewe, basi sio matokeo ambayo yatairejesha Israel kwenye mkondo sahihi."
Msaidizi mkuu wa Rais wa Palestina Mahmoud Abbas ameyashutumu mafanikio hayo yanayotabiriwa ya Netanyahu, akisema kuwa unyakuzi wa maeneo ya Ukingo wa Magharibi unaokaliwa umepata ushindi.
Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Palestina – PLO Saeb Erakat amesema katika taarifa kuwa Netanyahu ameamuwa kuwa muendelezo wa kuikalia ardhi ya Wapalestina na mzozo ndicho kinacholeta maendeleo na ustawi nchini Israel, na kwa hiyo amechagua kuimarisha misingi na nguzo za mgogoro huo na mzunguko wa machafuko, itikadi kali, vurugu na umwagaji damu. Hatua inayofuata ni unyakuzi. Amesema Erakat.