1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEC yavitaka vyama kuwasilisha majina ya mawakala

16 Oktoba 2020

Tume ya uchaguzi Tanzania - NEC, imevitaka vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi kuhakiikisha vinawasilisha majina ya mawakala wao katika vituo vya kupigia kura siku saba kabla ya zoezi hilo kuanza kufanyika

https://p.dw.com/p/3k0zS
Tansania Dodoma | Headquater | Uchaguzi House Tanzania
Picha: DW

Tume ya taifa ya uchaguzii imezungumza hayo wakati wakikabidhi daftari la kudumu la wapiga kura kwa vyama vya siasa, ambalo litatumika pia na vyama hivyo katika kuwapanga mawakala wao ambao watakuwa wakiratibu zoezi zima la kupiga kura na kuhesabu kura ambazo wagombea kutoka katika vyama vyao wamezipata katika zoezi hilo la kidemokrasia. Soma pia: Magufuli kuhitimisha kampeni za Dar es Salaam

Akinukuu kifungu cha 57 katika sheria ya taifa ya uchaguzi mkurugenzi wa uchaguzi kutoka NEC bwana Charles Mahera amesema, sheria hiyo imetoa maelekezo kuwa, vyama vya siasa vitatakiwa kuwasilisha majina ya mawakala siku saba kabla ya zoezi la kupiga kura, hivyo kuvitaka vyama hivyo kuwasilisha majina kwa wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo mnamo Oktoba 21na si vinginevyo.

Afrika Tansania Präsidentschaftswahlen 2020
Watanzania watawachagua viongozi wapya Oktoba 28Picha: DW/S. Khamis

Ufafanuzi huu umetolewa kutokana na baadhi ya vyama vya siasa kupata taharuki kuwa kuna baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi walianza kutoa utaratibu wa kuwasilishwa kwa majina ya mawakala wa vyama vya siasa kabla ya wakati unaoelekezwa kwa mujibu wa sheria jambo ambalo, mkurugenzi Mahera amelitaja kuwa ni kinyume na utaratibu na badala yake majina hayo yawasilishe siku saba kabla ya uchaguzi. Soma pia: Kampeni Tanzania zaingia ngwe ya lala salama

Baadhi ya vyama vya siasa ambavyo mara kadhaa vimekuwa vikitaja kupata usumbufu kutoka kwa wasimamizi wa uchaguzi katika kutekeleza zoezi hilo vimesema, tayari wamejipanga kuhakikisha wanafuata utaratibu ili wapate uwakilisha katika zoezi hilo na kuwataka wasimamizi hao kutoleta vikwazo wakati mchakato huo ukiendelea. Walisisitiza

Kadhalika mkurugenzi huyo wa uchaguzi ameukumbusha umma na wadau wa uchaguzi kuwa, jukumu la kutangaza matokeo ya uchaguzi ni la tume hiyo ya uchaguzi na si la upande mwingine wowote, hivyo haitamvumilia yeyote atakaeipora madaraka yake iliopewa kwa mujibu wa katiba. Soma pia: Upigaji kura wa mapema Zanzibar wazua minong'ono

Takriban siku kumi na moja zimesalia hadi Tanzania kuingia kwenye uchaguzi wake wa sita tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi  zaidi ya miongo miwili iliyopita.

Mwandishi: Hawa Bihoga DW, Dar es salaam