Ndugu wa familia wenye ushawishi Afrika
Barani Afrika katika siasa mara nyingi utakuta ni mambo ya familia: mwana kumrithi baba katika urais, binti kuongoza mashirika, mke ni waziri. Fuatilia taarifa hii katika matukio ya picha.
Mtoto wangu, mlinzi wangu
Muhoozi Kainerugaba ni mtoto wa kwanza wa rais wa muda mrefu wa Uganda Yoweri Museveni. Ni afisa mwandamizi katika jeshi la Uganda akiongoza kitengo maalumu chenye wajibu wa kumlinda Rais. Mke wa Museveni Janet ni Waziri wa Elimu na Michezo katika Baraza la Mawaziri. Shemeji yake Rais Museveni, Sam Kutesa, ni waziri wa mambo ya kigeni.
Binti wa rais aliye Bilionea
Isabel dos Santos, ni binti wa kwanza wa rais wa Angola, ni mmoja wa waafrika10 tajiri. Himaya yake ya biashara ni pamoja na umiliki wa kampuni kubwa ya simu nchini humo na mlolongo wa maduka makubwa. Ni mkuu wa kampuni ya mafuta ya taifa ya Sonangol. Kaka yake José Filomeno anaongoza mifuko ya uwekezaji na rasilimali ya taifa nchini Angola FSDEA ambayo ina utajiri wa zaidi ya dola bilioni tano.
Baba yangu, anatawala
Teodoro Nguema Obiang Mangue ni makamu wa pili wa rais wa Guinea ya Ikweta - na wakati huo huo ni mtoto wa rais. Baba yake, Teodoro Obiang Nguema Mbasogo, ametawala nchi hiyo tangu mwaka 1979. Wakati huo huo mtoto wake wa kufikia, Gabriel Mbega Obiang, ni Waziri wa mafuta. Kampuni ya mafuta ya GEPetrol iliongozwa na ndugu wa Rais, Nsue Okomo hapo awali.
Dada mwenye ushawishi mkubwa
Jaynet Desiree Kabila Kyungu ni binti wa rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Laurent Kabila. Kaka yake ambaye ni pacha ndiye rais wa sasa Joseph Kabila. Jaynet ni mbunge na pia anamiliki mojawapo ya kampuni kubwa ya habari. Katika nyaraka zilizovuja za "Panama" ilibainika kwamba alikuwa mwenyekiti mwenza wa kampuni ya nje iliyo na hisa katika kampuni kubwa ya simu nchini Congo.
Kutoka ukatibu muhtasi hadi mke wa rais
Grace Mugabe ni mke wa pili wa kiongozi wa muda mrefu wa Zimbabwe Robert Mugabe. Wawili hao walianza mahusiano wakati alipokuwa msaidizi wake. Wakati huo huo Grace ni mwenyekiti wa baraza la wanawake katika chama tawala tawi lenye ushawishi mkubwa. Ingawa ana umri wa miaka 51 anaonekana kama mrithi wa mume wake mwenye miaka 92 atakapoondoka madarakani.
Mke wa zamani mwenye uchu mkubwa
Nkosazana Dlamini-Zuma ni mwanamke wa kwanza kuchaguliwa mkuu wa Umoja wa Afrika. Hapo awali aliwahi kuwa waziri wa mambo ya nje wakati wa utawala wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki na Waziri wa Mambo ya Ndani katika serikali ya mume wake wa zamani, Jacob Zuma. Ndoa yao ilivunjika kabla ya yeye kuwa waziri.
Utaifa, biashara ya familia
Makampuni mengi na muhimu na nafasi za juu katika siasa ziko mikononi mwa familia ya Denis Sassou Nguesso, Rais wa Jamhuri ya Kongo. Binti yake Claudia (pichani) anaongoza idara ya mawasiliano ya baba yake, ndugu yake Maurice anamiliki makampuni mbalimbali na mwana mwingine wa rais Denis Christel anatajwa kuwa tayari kumrithi baba yake.
Rais Bongo, wa pili
Kwa miaka 41 Omar Bongo Ondimba ameitawala Gabon. Alifariki akiwa madarakani mwaka 2009. Katika uchaguzi uliozua utata katika duru ya kwanza mtoto wake, Ali Bongo alijipatia kura na kuwashinda wagombea wengine 17 wa upinzani. Mwaka 2016 aliapishwa na kuthibitishwa kuchukua madaraka. Ikimaanisha familia ya Bongo imetawala kwa nusu karne.
Kama baba, kama mwana
Kati ya takriban watoto 50 wa Rais wa zamani wa muda mrefu wa Togo Gnassingbé Eyadéma, Faure Gnassingbé alikuwa ni mtoto pekee aliyejiingiza katika siasa. Hivi sasa ndiye anayeliongoza taifa hilo. Pia nchini Kenya na Botswana kwa sasa marais walioko madarakani ni watoto wa marais wa zamani wa mataifa hayo