Ndege za NATO zafanya mashambulizi ya angani Misrata na Ajdabiya
10 Aprili 2011Mashambulizi ja ya jumuiya ya NATO yamesaidia kuzuia hararkati kubwa ya vikosi vya Gadhafi dhidi ya mji wa Ajdabiyah, unaidhibitiwa na waasi. Jumuiya ya NATO imesema imeviharibu vifaru 11 nje ya mji huo na vingine 14 katika mji wa Misrata, ngome pekee ya waasi magharibi mwa Libya ambayo imekuwa ikizingirwa kwa wiki sita zilizopita. Hali ya maisha inaripotiwa ngumu kwa raia wa mji huo.
Mapema leo waasi walionekana wakipoteza udhibiti wa mji wa Ajdabiyah kufuatia operesheni kubwa ya vikosi vya serikali dhidi yao ambayo imekuwa ikiendelea kwa takriban wiki nzima. Uvamizi huo ulijumuisha mashambulizi makali ya mabomu na makombora kuanzia Jumamosi wili iliyopita, huku wanajeshi wa Gadhafi wakiingia ndani ya mji huo.
Kwa saa kadhaa waasi walijificha kwenye barabara za mji wa Ajdabiyah, ambao ni njia yao muhimu kelekea ngome yao huko mjini Benghazi, kilometa 150 kuelekea pwani ya bahari ya Meditereania.
Maiti za waasi wanne zilionekana zikiwa zimetupwa kando ya barabara. " Koo zao zilikuwa zimekatwa. Wote walikuwa wamepigwa risasi mara kadhaa kifuani pia. Sikuweza kujizuia kulia wakati nilipoiona. Mambo yanazidi kuwa magumu mno," amesema mmoja wa waasi, Muhammad Saad.
Viongozi wa Umoja wa Afrika wawasili
Wakati huo huo ujumbe wa ngazi ya juu wa Umoja wa Afrika ukiongozwa na rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, umewasili mjini Tripoli leo kujaribu kuanzisha mazungumzo ya amani kati ya pande zinazohasimiana. Maafisa wa Afrika Kusini wamesema ujumbe huo unawajumuisha pia marais Ould Abdel Aziz wa Mauritania, Amadou Toumani Toure wa Mali na Denis Sassou Nguesso wa Jamhuri ya Kongo. Watakutana na waasi katika mji wa Benghazi baada ya kukutana na Gadhafi mjini Tripoli.
Maafisa nchi za magharibi wametathmini kuwa nguvu za kijeshi hazitafaulu kuwasaidia waasi kumuondoa kwa nguvu madarakani kanali Gadhafi na sasa wanasisitiza suluhisho la kisiasa. Lakini msemaji wa waasi amekataa kufanyika kwa mazungumzo yoyote. Amesema hakuna suluhu nyengine kwa kuwa lugha ya Gadhafi ni umwagaji damu na watu wanaoizungumza lugha hiyo ndio wanaoielewa.