1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya utulivu yarejea katika uwanja wa ndege wa Kabul

Sylvia Mwehozi
17 Agosti 2021

Ndege za kijeshi zinazowabeba wanadiplomasia na raia kutoka Afghanistan zimeanza tena safari zake mapema leo, siku moja baada ya maelfu ya watu kuvamia uwanja wa ndege wa Kabul kwa matumaini ya kukimbia nchi,

https://p.dw.com/p/3z4ic
Afghanistan Bildergalerie Kabul Flughafen Evakuierung
Picha: WAKIL KOHSAR/AFP

Ripoti zinasema kuwa idadi ya raia imepungua katika uwanja wa ndege wa Kabul siku moja baada ya kutokea tafrani wakati maelfu ya watu walipouvamia uwanja huo wa ndege kwa matumaini ya kukimbia nchi. Wanajeshi wa Marekani walijaribu kutawanya umati huo kwa kufyatua risasi huku wengi wao wakijaribu kuning'inia katika ndege ya kijeshi ya Marekani wakati ikianza kuondoka.

Hali hiyo ilisababisha safari za ndege kusitishwa Jumatatu wakati watu watano walipouawa ingawa haikuwa wazi ikiwa walipigwa risasi au walikufa kwa sababu ya mkanyagano. Ripoti nyingine za vyombo vya habari zinasema kuwa watu wawili walianguka kutoka pembeni mwa ndege hiyo baada ya kupaa na kufariki.

Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imesema ndege yake ya kijeshi iliyoondoka Kabul Jumatatu jioni ilifanikiwa kuwabeba watu saba tu. Msemaji huyo aliongeza kuwa "hapakuwa na uhakika jana usiku kwamba raia zaidi wa Ujerumani na watu wengine wanaotakiwa kuhamishwa kama wangeweza kufika uwanja wa ndege bila ya ulinzi wa wanajeshi wa Ujerumani". Mwandishi mmoja wa Afghanistan ameripoti kuwa baadhi ya shughuli zimeanza kurejea kawaida.

Afghanistan Kabul Flughafen Evakuierungen Chaos
Raia wa Afghanistan wakikimbilia ndege ya kijeshi ya MarekaniPicha: AP Photo/picture alliance

"Nimetembea katika maeneo ya mjini asubuhi hii na kuna ulinzi wa Taliban katika majengo ya serikali kama ikulu na wizara ya ulinzi. Kwa nyongeza ni kuwa baadhi ya maeneo ya umma yamefunguliwa. Shule zimeanza masomo na taasisi nyingi za umma zimefunguliwa tena. Kila mmoja anapenda amani na utulivu wa kudumu na wana matumaini kwamba kila upande utajiunga katika serikali ambayo ni jumuishi".

Wakati huo huo kundi la Taliban limetangaza "msamaha" kote Afghanistan na kuwahimiza wanawake kujiunga na serikali yake na kujaribu kutuliza hali katika mji mkuu wa Kabul baada ya ghasia zilizoshuhudiwa katika uwanja wa ndege. Kauli hiyo imetolewa na Enamullah Samangani, mwanachama katika tume ya kitamaduni ndani ya Taliban, ikiwakilisha maoni ya kwanza juu ya uongozi.

Hayo yakijiri mazungumzo yanaonekana kuendelea baina ya Taliban na maafisa kadhaa wa serikali ya Afghanistan, akiwemo rais wa zamani Hamid Karzai na Abdullah Abdullah ambaye wakati mmoja aliwahi kuongoza baraza la majadiliano. Afisa mmoja ambaye anafahamu moja kwa moja juu ya mazungumzo hayo, aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina alisema kiongozi wa Taliban Amir Khan Muftaqi amewasili mjini Kabul akitokea Qatar. Muftaqi ni waziri wa zamani wa elimu wakati wa utawala wa mwisho wa Taliban na alianza kufanya mazungumzo na viongozi wa kisiasa wa Afghanistan hata kabla ya rais Ashraf Ghani aikimbie nchi.