1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege za kijeshi zarejelea safari zake Kabul

17 Agosti 2021

Hali ya utulivu imerudi katika uwanja wa ndege wa Kabul baada ya vurugu za jana katika uwanja huo zilizoshuhudia mamia ya watu wakijaribu kuikimbia nchi hiyo baada ya Taliban kuchukua madaraka.

https://p.dw.com/p/3z4fo
Afghanistan | Evakuierung von Afghanen aus Kabul durch die U.S. Air Force
Picha: Courtesy of Defense One/REUTERS

Ndege za kijeshi zinazowaondoa watu kutoka kabul pia zimerejelea safari zake nchini humo. 

Mamia ya watu walimiminika katika uwanja wa ndege wa Kabul jana Jumatatu baada ya Taliban kuuteka mji mkuu wa Kabul, wenye idadi ya watu milioni 5 na kuiondoa madarakani serikali inayoungwa mkono na mataifa ya Magharibi.

Hakuna ripoti za machafuko leo Jumanne, lakini wakaazi wengi wamesalia majumbani wakiwa na hofu baada ya Taliban kuwaachilia huru wafungwa na silaha kuporwa.

Rais Joe Biden wa Marekani ametetea uamuzi wake wa kuviondoa vikosi vya jeshi la Marekani na kuonyesha masikitiko ya jinsi hali ilivyo mjini Kabul.