Nchi za Ulaya zakubali mkataba wa Iran una mapungufu
17 Mei 2018Mara baada ya kuwasili katika mkutano huo wa kilele mjini Sofia, Bulgaria Merkel amesema kwamba,
"kila mtu katika umoja wa Ulaya anakubaliana na mtizamo kwamba makubaliano hayakuwa kamilifu, lakini tunapaswa kusalia katika makubaliano haya na kufanya majadiliano zaidi na Iran kwa misingi ya masuala mengine kama vile programu ya makombora ya masafa marefu."
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaohudhuria mkutano huo wa kilele wamekubali kuwa na mshikamano wa kuyaendeleza makubaliano ya nyuklia na Iran baada ya rais Donald Trump kujiondoa na kuiwekea vikwazo tena Iran, akilalamika kwamba makubaliano hayo hayakufanya lolote kuzuia programu ya makombora ya masafa marefu ya nchi hiyo au kuingilia kati katika mgogoro wa mashariki ya kati.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema umoja huo unapigana kuulinda mkataba huo ili biashara na Iran iweze kubakia. Macron amesema jitihada hizo zitakwenda sambamba na kazi ya kutafuta majadiliano juu ya makubaliano muhimu, akiongeza kwamba mkataba wa mwaka 2015 unapaswa kukamilishwa na makubaliano ya nyukilia ya 2025, kukubaliana juu ya shughuli za makombora ya masafa marefu na uwepo wa Iran kikanda.
Tehran imeonya kwamba imejiandaa kuanza tena mchakato wa "viwanda vikubwa", uboreshaji wa uranium bila ya "vikwazo vya aina yoyote" labda kama Ulaya itatoa dhamana kwamba itadumisha faida za kiuchumi zilizopatikana kutokana na makubaliano ya nyuklia licha ya Washington kurejesha vikwazo.
Wataalamu wa Umoja wa Ulaya wameanza kuweka hatua za kuulinda mkataba huo kutoathirika na vikwazo vya Marekani, wakilenga katika masuala muhimu tisa ikiwa ni pamoja na Iran kuuza bidhaa zake za mafuta na gesi pamoja na kufikia fedha za kimataifa.
Lakini kutokana na athari za kidunia za vikwazo vya serikali ya Marekani haijulikani jinsi hatua hizo zinaweza kufanya kazi, au kama Umoja wa Ulaya utajaribu kuwatumia kama mpango wa biashara na Washington.
Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk amemkosoa vikali Rais wa Marekani na kusema Ulaya imshukuru Rais Trump kwa kuwagutua kwamba walikuwa wakijidanganya, na kwamba hatua ya Trump imewafanya watambue lazima wajisaidie wenyewe bila ya Marekani.
"Bara la Ulaya ama litakuwa eneo lenye ushawishi au kibaraka. Ulaya lazima ishikamane kiuchumi, kisiasa na kijeshi kuliko ilivyokuwa zamani. Kwa ufupi ama tushikamane pamoja au hatutakuwa chochote," amesema Tusk.
Mkuu wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Junker, aliwasilisha suluhisho kadhaa za kuweza kulinda uwekezaji wa Ulaya nchini Iran na pole pole kufufua ushirikiano wa kiuchumi, ambao mataifa mengi ya Ulaya wanatarajia kunufaika nao ikiwa ni pamoja na kuiruhusu Benki ya Uwekezaji ya Ulaya kuwekeza nchini Iran.
Vile vile viongozi hao wameunga mkono mpango wa pamoja wa kukabiliana na kitisho cha Trump cha kodi juu ya bidhaa za za chuma zinazouzwa Marekani kutoka Ulaya, wakisema kamwe Ulaya haitafanya mazungumzo chini ya vitisho.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/afp/reuters/ap
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman