1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Libya lapongezwa kwa kuipitisha serikali ya umoja

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
12 Machi 2021

Nchi za Ulaya, Marekani, Misri na Jordan zimelipongeza bunge la Libya kwa kuipitisha serikali ya umoja kwa ajili ya kuliongoza taifa hilo hadi utakapofanyika uchaguzi mwezi Desemba.

https://p.dw.com/p/3qWgn
Libyen Parlament
Picha: Esam Omran Al-Fetori/REUTERS

Kwenye taarifa yao ya pamoja, mawaziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Ufaransa, Marekani, Italia na Uingereza wamewapongeza watu wa Libya kwa azma yao ya kuurudisha umoja nchini mwao na wametoa wito wa kuondolewa wapiganaji wote wa kigeni na mamluki kutoka nchini Libya. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas, amesema nchi yake imefurahishwa mno na hatua iliyofikiwa nchini Libya. Maas amesema kupitia mchakato wa Berlin, Ujerumani na washirika wake wataendelea kuwaunga mkono watu wa Libya na juhudi za Umoja wa Mataifa.

Najla el-Mangoush, aliyechaguliwa kuwa mwanamke wa kwanza kuwa waziri wa mambo ya kigeni, ataapishwa wiki ijayo kama sehemu ya serikali mpya ya umoja. Ni jambo adimu nchini Libya kwa mwanamke kuwa kwenye ngazi ya juu serikalini, na uteuzi wa Bi Najla el-Mangoush umepokelewa vizuri na kupongezwa na wanawake wengi wa Libya.

Waziri Mkuu wa Libya Abdul Hamid Dbeibeh
Waziri Mkuu wa Libya Abdul Hamid DbeibehPicha: Mucahit Aydemir/AA/picture alliance

Wakili huyo, ambaye pia alikuwa miongoni mwa waliokuwa na majukumu katika kipindi cha baraza la mpito lililotawala kwa muda mfupi nchini Libya baada ya ghasia za mwaka 2011, ataungana na wanawake wengine wanne katika baraza jipya la mawaziri, akiwemo Halima Abdulrahman atakayehudumu kama waziri wa sheria.

Serikali ya mpito ya Waziri Mkuu Abdulhamid Dbeibeh imepatikana baada ya mchakato wa mazungumzo yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa na sasa imepewa jukumu la kuziunganisha taasisi za serikali zilizogawanyika nchini Libya na hatimaye kusimamia uchaguzi wa mwezi Desemba.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani  Heiko Maas
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko MaasPicha: Ludovic Marin/REUTERS

Wajumbe 75 wa Libya walichaguliwa na Umoja wa Mataifa kushiriki katika mazungumzo hayo na walitoa ahadi kwamba serikali mpya itawajumuisha wanawake kwa kiwango cha asilimia 30 kwa kuwapa majukumu ya juu serikalini, zikiwemo nafasi katika baraza la mawaziri.

Kwa Libya iliyokuwa imegawanyika, mafanikio ya uteuzi wa serikali ya umoja yameongeza matumaini ya kupatikana amani na maridhiano baina ya watu wa taifa hilo waliochokeshwa na vurugu na machafuko yaliyodumu kwa muongo mzima.

Vyanzo: AFP/RTRE