1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za SADC zatakiwa kupambana na makundi yenye silaha

21 Mei 2021

Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC zimetakiwa kuunganisha nguvu na kushirikiana kupambana na vikundi vyenye silaha ili kustawisha na kuimarisha hali ya usalama wa watu wake.

https://p.dw.com/p/3tmdp
Logo von SADC

Hayo yamebainishwa siku ya Ijumaa katika kongamano lililoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nchini Tanzania wakijadili kama nchi wanachama mafanikio na changamoto za SADC katika kipindi cha miongo minne sasa.

Tanzania inaona kwamba kuna haja mataifa hayo 16 yaliyo ndani ya jumuiya yashirikiane kwa dhati kuondoa vikundi vyenye silaha na mlengo wa kigaidi ambavyo vimeendelea kusumbua baadhi ya nchi kama vile Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Msumbiji.

Meja Jenerali Ibrahim Muhona ambaye ni mtaalamu wa masuala ya usalama katika ukanda huo amesema kutokuwepo kwa utulivu katika baadhi ya mataifa wanachama kunatokana na vikundi vya kigaidi kuendelea kusumbua katika baadhi ya maeneo hatua inayosababisha baadhi ya watu kuyahama makaazi yao na kutafuta hifadhi kwengineko.

Tanzania yanyooshewa kidole

Majadiliano haya yanafanyika ikiwa Tanzania ni miongoni mwa wanachama wenye nguvu katika jumuiya hiyo ambapo imekuwa ikinyooshewa kidole na jumuiya za kimataifa kutokana na uamuzi wake wa kuwarudisha nyuma waomba hifadhi kutoka Msumbiji wasiopungua 1,500 baada ya kukimbia mashambulio mabaya kutoka kwa vikundi visivyo vya serikali na vyenye mlengo wa kigaidi ambavyo vimeonekana kushamiri na kuleta wasiwasi na kuwafanya watu kuyahama makazi yao. 

Soma zaidi: Wakuu wa SADC walaani uasi Msumbiji

Kando na suala la usalama, hoja ya vijana wanaotafuta maisha bora kwa kuhama kutoka taifa moja kwenda jingine ndani ya jumuiya hiyo, hukumbana na visa vya ukatili hata mauaji, mataifa yametakiwa kuchukua hatua ya kuelimisha wananchi wao ili jumuiya kuwa salama na huru kwa kila mmoja. Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete alikuwa miongoni mwa wachangiaji wakuu wa mjadala huo.

Hata hivyo, wachambuzi wa mambo wanasema SADC ni miongoni mwa jumuiya zilizo imara barani Afrika na imefaulu katika siasa zake madhubuti, kitamaduni huku wakisisitiza kuna haja ya kuongeza nguvu ya pamoja ili kuleta mafanikio makubwa katika sekta ya uchumi kulingana na rasilimali zinazopatikana katika jumuiya hiyo.